Jumaa aipa kongole Simba
Na Omary Mngindo, Mlandizi
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitia Jumuiya ya Wazazi, MNEC Humoud Jumaa, ameipongeza klabu ya soka ya Simba kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho.Aidha, Jumaa amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa chachu kubwa ya klabu hiyo kutinga fainali, kutokana na mchango wake wa ndege na malazi wakati wakiwa nchini Afrika Kusini.
"Tunaipongeza klabu ya soka ya Simba kwa kumheshimisha Rais Dkt. Samia, kwani kitendo cha kuipatia usafiri pamoja na malazi kiliiongezea hamasa, endapo isingefaulu ingekuwa aibu kwa taifa," alisema Jumaa.
Sanjali na hilo, amempongeza Naibu Waziri wa Michezo Hamisi Mwinjuma, kwa kusafiri mpaka nchini humo, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Rais kwani uwepo wake uliwaongezea chachu zaidi wachezaji.
"Baada ya matokeo ya mchezo wa awali, Naibu Waziri Mwinjuma aliwatia moyo wachezaji, kufuatia ushindi mwembamba wa bao 1-0, aliwahamasisha na kuwatuliza wanamichezo kuelekea mechi ya marudiano," alisema MNEC huyo.
Aliongeza kuwa, "Kwa hatua iliyofikiwa na hamasa inayoendelea kutolewa na Serikali chini ya mwanamichezo namba moja nchini Dkt. Samia Suluhu nina imani kubwa ubingwa utatua nchini," alisema Jumaa.
Jumaa alimalizia kwa kuwataka waTanzania kuondoa tofauti za Usimba na Uyanga, badala yake kwa pamoja waiombee dua timu hiyo ili iweze kuandika historia ya kutwaa ubingwa huo.
Pia, amempongeza mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Mohamed Dewj (MO) kwa ufadhili anaouendeleza kwani matunda ya uwekezaji huo yanazidi kuonekana, huku akiwaomba wana Simba kuendeleza umoja, amani, upendo na mshikamano.
No comments