Header Ads

ad

Breaking News

TPA kuwapunguzia kodi waathirika janga la ghorofa Kariakoo

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) itawapunguzia gharama za uhifadhi mizigo waathirika wa jengo la ghorofa lililoporomoka katika soko  Kariakoo jijini Dar es Salaam Novemba 16, 2024.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus,  alitoa ahadi hiyo hapa jana  kwa waandishi wa habari  na kueleza kwamba TPA ina utaratibu wa kuwapunguzia gharama za uhifadhi wa mizigo waathirika wa majanga ambao ni wateja wa bandari.

Alifafanua kwamba utaratibu wa kuwapa nafuu wadau  waliopatwa na majanga pale wanapotoa taarifa zenye mashiko ni wa kawaida na imeshafanya hivyo mara kadhaa kwa utaratibu huu.

 “Kuna janga na janga. Lipo janga mtu ataondolewa na tozo ya asilimi 50; kuna majanga mengine, kulingana na ukubwa, mdau anaweza kuondolewa tozo kabisa.”

Mfanyabiashara atatakiwa  kutoa taarifa ya janga liliomkuta kwa wakala wake wa forodha  na  wakala atawasilisha taarifa hiyo TPA. 

Alieleza kwa mantiki hiyo, waathirika wa janga la Kariakoo wasiwasiliane na TPA moja kwa moja, bali wawasiliane na mawakala wao. 

 “Kwa utaratibu wetu tunahifadhi bure mzigo wa mfanyabiashara bandarini kwa siku tano tu. Baada ya hapo mfanyabiashara atatozwa kodi ya mzigo wake kulingana na siku mzigo huo utakapokaa bandarini,” alifafanua.

Pia amesema kuwa TPA inawapa pole wafanyabiashara waliokutwa na tukio hilo, wakiwa kama wadau wakuu wa bandari hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa aliyopewa Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Jumatano alipotembelea eneo hilo, watu 20 walikuwa wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa na kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa jijini.

Sababu ya kuanguka kwa jengo hilo bado haijafahamika, ambapo tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa maagizo ya Rais Samia ameunda tume maalum kwa ajili ya ukaguzi wa majengo katika eneo hilo  kuu la  biashara ili kuepuka maafa katika siku za usoni

No comments