PPRA yaokoa bilioni 14.94 kwa kutumia mfumo wa NeST
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba akiwasilisha wasilisho wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jana jijini Dar es Salaam, leo Novemba 4,2024.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA), imesema katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 imeokoa Sh bilioni 14.94 kupitia ukaguzi na Sh trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji.
Akizungumza jana katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu, Dennis Simba, anasema PPRA chini ya Wizara ya Fedha hadi Oktoba 31,2024 jumla ya taasisi nunuzi 21,851 zimesajiliwa na zinatumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).
Simba anasema kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina Na.370 na marekebisho yake na sheria nyingine zinazoongoza, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina mamlaka ya kusimamia shughuli zote na rasilimali zote za mashirika ya umma.
Pia Msajili wa Hazina ana mamlaka ya kusimamia taasisi na wakala wa Serikali na kupitia matumizi ya fedha katika mashirika ya umma na yaliyoundwa kisheria kwa lengo la kuendeleza hatua zinazolengwa kuunganisha, kuvunja au kuboresha utendaji wake.
Simba anasema chini ya uongozi wa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan, bajeti ya ununuzi ya ziadi ya Sh trilioni 38.6 imewekwa kwenye mfumo wa NeST, ambayo ni fursa ya wazi kwa ajili ya wazabuni.
Mkurugenzi Mkuu huyo anasema wazabuni zaidi ya 28,590 wamesajili kwenye mfumo wa NeST, wakati mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 10.2 imetolewa kwa wazabuni kupitia mfumo huo.
Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani Vicky Molle akitoa wasilisho katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, jana jijini Dar es Salaam, leo Novemba 4,2024
“Ununuzi wa umma ni shughuli muhimu ya kiuchumi inayohusisha sehemu kubwa ya Pato la Taifa (GDP), takriban asilimia 70 ya bajeti ya Serikali na taasisi zake hutumika kwenye ununuzi wa umma ambao unasimamiwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410.
Anaongeza kuwa, chini ya sheria hiyo zimeundwa kanuni za Ununuzi wa Umma 2024 na miongozo kwa ajili ya kuweka taratibu za ununuzi wa umma, ambapo kanuni mpya za Ununuzi wa Umma zimekamilika.
“Mamlaka imewezesha ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi kwa kuanzisha kanda sita katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Tabora, Arusha na Mtwara.
Mkurugenzi Mkuu huyo anasema PPRA wamekamilisha ujenzi wa ofisi ya makao makuu na kuhamia tangu Machi 2024, kitendo ambacho kimesaidia kuokoa fedha ambayo ungepelekwa kulipia kodi ya pango.
“Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma imetoa fursa kwa wazabuni wa ndani kushirikiana na wazabuni wa nje (partnership), kampuni ya ndani ndiyo itakayokuwa kiongozi na fedha zitalipwa kupitia kampuni ya ndani.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano Sabato Kosuri akifafanua jambo wakati wa kikao kazi leo Novemba 4,2024 jijini Dar es Salaam
Simba anasema kuwa, zabuni zenye thamani ya isiyozidi Sh bilioni 59 zimetengwa kwa ajili ya wazabuni wa ndani ya nchi, ambapo mfumo wa NeST umekuwa na mchango mkubwa kusimamia suala hilo kwa ufanisi sana.
Anaongeza kuwa, sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 inazitaka taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu ambapo Mfumo wa NeST kama nyenzo, umesaidia utekelezaji wake.
Simba anaongeza kuwa, tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa NeST Julai 1 mwaka jana hadi Oktoba 8, mwaka huu jumla ya vikundi 210 (makundi maalum), vimefanikiwa kupata tuzo za zabuni zenye jumla ya thamani zaidi ya Sh bilioni 9.856.
Anasema katika Mwaka wa Fedha Julai 1,2023 hadi Juni 30, 2024, vikundi 85 vya vijana vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.9.
Mkurugenzi Mkuu huyo anasema makundi mengine kuanzia Julai 1,2023 hadi Juni 30,2024, vikundi 84 vya wanawake vilipata zabuni zenye thamani ya zaidi Sh bilioni 4, wakati vikundi viwili vya wazee vikapata zabuni zenye thamani ya Sh milioni 74.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akitoa neno la shukrani baada ya wasilisho leo Novemba 4,2024, leo Novemba 4,2024 jijini Dar es Salaam
Simba anataja majukumu ya PPRA kuwa ni pamoja na kutoa miongozo chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, kuratibu na kutunza Mfumo wa Uchapishaji wa Taarifa kuhusu Fursa za Ununuzi wa Umma, Tuzo na Taarifa nyingine zozote zenye maslahi kwa umma kama itakavyoamuliwa na Mamlaka.
Jukumu lingine analolitaja ni kufanya ukaguzi kwa vipindi maalum wa kumbukumbu na mienendo ya taasisi nunuzi ili kuhakikisha matumizi kamili na sahihi ya Sheria hii.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba (katikati), akisikiliza maswali. Wa kwanza kushoto ni Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani Vicky Mollel na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile
Anaongeza kuwa, matokeo ya fursa katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.10 ya Mwaka 2023 yanayotarajiwa kupatikana katika fursa hizo ni pamoja kuimarika na kukua kwa viwanda vya ndani, kuongezeka kwa ajira na Pato la Taifa na kubadilishana uzoefu na ujuzi baina ya wataalamu wa ndani na wataalamu wa nje kupitia mikataba mbalimbali.
Mengine ni kupungua kwa gharama za ununuzi, kuimarika kwa sekta binafsi na makundi maalumu ya kijamii na kuongezeka kwa ushiriki wa wazabuni na ushindani, ambapo itasaidia kuimarisha uwazi, uwajibikaji, ufanisi na hivyo kupata thamani halisi ya fedha iliyotumika kupitia shughuli za ununuzi wa umma na ugavi.
Kuhusu ununuzi wa bidhaa na huduma mtambuka, Mkurugenzi Mkuu huyo anasema mfumo unampa nafasi mzabuni kujisajili kwenye “business lines” zenye kumwezesha kushiriki kwenye zabuni za CUIS.
Anasema baada ya kujisajili, mzabuni atatakiwa kukubaliana na masharti na vigezo (Terms and Conditions) kwa kusaini nyaraka ndani ya mfumo ya kushiriki kwenye zabuni za CUIS.
"Taasisi za Umma zitakuwa na uwezo wa kutangaza zabuni za CUIS na kuwa na uwezo wa kuchagua eneo (wilaya, mikoa, au nchi nzima) ambapo anataka wazabuni wapate mualiko wa kushiriki kwenye zabuni," anasema Simba.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahairi Tanzania (TEF), Anitha Mendoza akisikiliza kwa makiniKuhusu ununuzi mdogo mdogo, ambao thamani yake haizidi viwango vilivyoainishwa kwenye Kanuni za Ununuzi wa Umma, Simba anasema taasisi nunuzi zinapaswa kutumia njia ya ununuzi ya 'Micro Value Procurement' iliyopo kwenye Mfumo.
Anasema Ofisa wa Idara ataanzisha maombi ya ununuzi kwenye mfumo na yataidhinishwa hadi pale atakapopatiwa masurufu (imprest) na baada ya ununuzi kukamilika, Ofisa wa Idara aliyewasilisha maombi ya ununuzi atatakiwa kufanya mrejesho ndani ya mfumo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini kufungua akaunti ya mfumo wa NeST ili kupata matangazo.
Anasema kwa mfanyabiasha kutumia mfumo huo kunatoa fursa kubwa, kwani hata upande wa vyombo vya habari matangazo na zabuni nyingine zinapatikana kwa njia hiyo.
“Tuwapongeze kwa kurahisisha mfumo wa ununuzi katika nchi yetu, ndugu zangu wahariri, hata matangazo ya kwenye vyombo vya habari mengi yanapitia NeST, kwa hiyo sisi tunaoendesha vyombo vya habari kama huna akaunti ya NeST huwezi kufanikisha matangazo, hali ngumu ya vyombo vya habari tuliyonayo tuna nafasi ya kujikomboa kupitia kwenye mfumo huu,” anasesema Balile.
No comments