Header Ads

ad

Breaking News

Watoto saba kwenda kutibiwa nchini Israel

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter

Kisenge akizungumza na wazazi ambao watoto wao wanakwenda nchini Israel

kwaajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo wakati akiwaaga leo jijini Dar es Salaam.

Gharama za matibabu ya watoto hao saba na usafiri wa wazazi wao watano

pamoja na wataalamu wa JKCI wawili zinatolewa na Shirika la Okoa Moyo wa

Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel. 


Na  Stella Gama - Dar es Salaam


MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge ameishukuru Serikali ya Israel kupitia Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH), kuendelea kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji mgumu ambao haufanyiki hapa nchini.

 

Shukrani hizo amezitoa leo Septemba 11,2023 jijini Dar es Salaam wakati akiwaaga watoto saba na wazazi wao wanaokwenda nchini Israel leo jioni kwa ajili ya matibabu ya upasuaji mkubwa wa moyo.

 

Dkt. Kisenge alisema watoto hao wanaongozana na daktari bingwa wa moyo kwa watoto na muuguzi mmoja ambao watakuwa nao muda wote wa matibabu yao pamoja na kwenda kujifunza mambo mbalimbali kuhusu upasuaji huo ili watakaporudi nchini waweze kuwahudumia watoto wengine wenye matatizo ya moyo.

 

“Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu nachukua nafasi hii kuzishukuru serikali za Tanzania na Israel kwa kufadhili matibabu haya ya watoto.”

 

“Wenzetu Israel wametutangulia katika utaalamu wa upasuaji wa moyo kwani wameanza kufanya  upasuaji  kabla yetu, hivyo wanapokuja kufanya kambi za upasuaji wa moyo watoto ambao wanawakuta na matatizo yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi kuliko uliopo hapa nchini, wanawachukuwa na kwenda kuwafanyia upasuaji huo nchini kwao."

 

“Gharama zote za usafiri wa watoto, wazazi wao na wataalamu wetu wa afya na matibabu zinagharamiwa na SACH, ninawashukuru sana kwa moyo wao wa upendo walionao kwa watoto wetu wenye matatizo ya moyo na hii yote inatokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali za Tanzania na Israel,” alisema Dkt. Kisenge.

 

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Deogratius Nkya, ambaye anaambatana na watoto hao nchini Israel amesema wanatarajia kuondoka nchini leo jioni kuelekea Israel  kwa ajili ya matibabu ya watoto,  pia kujifunza mbinu mbalimbali za kuwahudumia  watoto mara baada ya kurejea hapa nchini.

 

Dkt. Nkya amezishukuru serikali za Tanzania na Israel kwa kutoa nafasi ya kuwasaidia watoto, na kutoa nafasi kwa wataalamu wa afya ya kuongozana na watoto hao kwani ni sehemu mojawapo ya kwenda kujifunza mbinu mbalimbali za upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto.

 

Naye, Jackline Patrick, mmoja wa wazazi ambao wanaongozana na watoto wao kwenda nchini humo, ameishukuru Serikali kwa kupata nafasi hiyo na kutoa kipaumbele katika kufanikisha kuwasafirisha watoto wao kwenda kupata  matibabu nchini Israel.

 

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inatibu magonjwa mengi ya moyo ya watoto kwa asilimia 90 kupitia wataalamu wazalendo waliopo. Hata hivyo wanamkataba  na Israel kwa baadhi ya wagonjwa wachache ambao ni asilimia 10 wanaohitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi kwenda kutibiwa nchii humo.



Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Deogratius Nkya akizungumza wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge akiwaaga watoto saba wanaokwenda kupatiwa matibabu nchini Israel kwa udhamini wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH).

Mzazi wa mtoto anayekwenda kutibiwa nchini Israel Jackline Mlay akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wazazi wenzake wakati wakiagwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kabla ya kuanza safari yao leo jijini Dar es Salaam. Gharama za matibabu ya watoto hao saba na usafiri wa wazazi wao watano pamoja na wataalamu wa JKCI wawili zinatolewa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaokwenda nchini Israel kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, wazazi wao pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo mara baada ya kuwaaga leo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI

No comments