NIC Insurance tumefanya vizuri katika soko-Dkt.Doriye
Na Frank Balile
SHIRIKA la Bima la NIC Insurance limepata mafanikio makubwa kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022, baada ya mabadiliko makubwa yaliyofanyika ili kujiimarisha zaidi Kibiashara, huku ikiwa ni kampuni ya kwanza ya bima kuanzishwa nchini.
Akizungumza leo Septemba 11,2023, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Insurance, Dkt.Elirehema Doriye, amesema kampuni hiyo imefanya mabadiliko mbalimbali ya Kiutendaji na Kibiashara kuanzia Julai, 2019 na kuweza kuingia kwenye ushindani ambao umewawezesha kufanya vizuri katika soko.
NIC Insurance ni kampuni inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, lengo lake kubwa ni kufanya biashara ya bima za mali, maisha na ajali, ikifanya vizuri zaidi ya makampuni 30 yaliyopo kwenye soko la bima nchini.
Amesema mabadiliko waliyofanya kwenye uongozi lengo lake ni kuongeza ufanisi, weledi na tija, huku wakiajiri wafanyakazi wenye uwezo na wabunifu.
Dkt.Doriye ameweka wazi kuwa, shirika hilo limefanya mabadiliko makubwa kwa kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya TEHAMA, ambayo imewawezesha kuongeza mapato na kupunguza muda wa kulipa madai.
"Tumefanikiwa kuondoa matumizi ya karatasi na kurahisisha utoaji wa huduma, tumefanikiwa kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 76.45, mwaka 2019 hadi 2020.
Amesema baada ya mabadiliko waliyofanya kuanzia mwaka 2019, wamefanikiwa kuondoa hasara kwa kuongeza mapato kutoka Shilingi Bilioni 76.45, mwaka 2019/2020, kiasi cha shilingi bilioni 103.94 mwaka 2021/22, sawa na asilimia 17.98 kwa mwaka.
“Tumelipa kodi ya mapato serikalini kutokana na faida tunayopata, ulipaji wetu umeongezeka kutoka shilingi bilioni 11.86 kwa mwaka 2019/20 hadi shilingi bilioni 15.14 kwa mwaka 2021/22, ikiwa ni wastani wa asilimia 13.80 kwa mwaka,” amesema Dkt. Doriye.
Dkt.Doriye amesema usimamizi mzuri wa matumizi na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi, kumechangia kuongeza ufanisi na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima, hivyo kuchangia kushusha gharama za uendeshaji na kuongeza faida kwa shirika.
NIC Insurance wamefanikiwa kulipa madai ya bima za wateja, ambapo hadi kufikia Juni 2022, wamelipa jumla ya shilingi bilioni 33.79, za bima ya maisha na shilingi bilioni 40.18 kwa bima za mali na ajali.
Dkt. Doriye alisema amesema faida ghafi imeongezeka kutoka shilingi bilioni 33.65 hadi shilingi bilioni 63.21, sawa na asilimia 43.91.
Wahariri wakisikiliza kwa makini
Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la NIC Insurance
Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la NIC Insurance
No comments