Header Ads

ad

Breaking News

ASKARI WA TAWA WAMWOKOA MTOTO WA TEMBO ALIYETUMBUKIA SHIMONI


Na Beatus Maganja, TAWA

ASKARI wa Hifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), jana Septemba 11, 2023, wamefanikiwa kumwokoa mtoto wa tembo anayekadiriwa kuwa na umri wa wiki nne,  aliyezama katika shimo lenye matope katika Kijiji cha Kwamsanja kilichopo Kata ya Kibindu  katika Halmashauri ya Chalinze jirani na Pori la Akiba Wamimbiki.

Taarifa za mtoto huyo wa tembo aliyetelekezwa na kundi lake na kutumbukia shimoni zilitolewa na raia mwema aitwaye Manase Thomas Baha, mkazi wa Kijiji cha Kwamsanja na kumlazimu Kamanda wa Pori la Akiba Wamimbiki, Emmanuel Lalashe, kutuma timu ya askari wanne walioshirikiana na askari wa Jeshi la Akiba (migambo) sita, kwa ajili ya kumwokoa mtoto huyo wa tembo.

Akizungumza baada ya uokoaji, Kamanda Lalashe aliwashukuru wananchi wanaoishi pembeni mwa Hifadhi ya Wamimbiki kwa ushirikiano wanaoutoa katika kulinda rasilimali za nchi zilizopo katika hifadhi hiyo, hususan rasilimali wanyamapori ambazo ni chachu ya shughuli za utalii na pato la nchi.

Mahusiano mazuri yaliyojengwa kati ya wahifadhi wa Hifadhi ya Wamimbiki na wananchi wanaoishi vijiji jirani na hifadhi hiyo, umekuwa na manufaa makubwa siku za hivi karibuni kwani wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa katika shughuli za uhifadhi.





No comments