Mikalanga mabingwa Kombe la Kahawa
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
TIMU ya soka ya Kata ya Mikalanga ya wilayani Mbinga mkoani Ruvuma imetwaa ubingwa wa Kombe la Kahawa (Kahawa Super 8 Cup), kwa mwaka 2023, baada ya kuifunga Nyasa United bao 1-0, katika mchezo uliokuwa na upinzani mkubwa.
Katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Edesius Kinunda, mkazi wa Dar es Salaam, lakini mzaliwa wa Magugu ikiwa na lengo la kuibua vipaji na kuviendeleza.
Bingwa wa mwaka huu alizawadiwa medali, kombe, kitita cha fedha taslimu shilingi sh.1,500,000, jezi seti mbili na mipira mitatu, wakati Nyasa United wao waliondoka na fedha taslimu shilingi 700,000, jezi seti mbili na mipira miwili.
Zawadi ya mshindi wa tatu ilikwenda kwa timu ya Mapera A, ambapo walizawadi fedha taslimu sh.300,000,jezi seti mbili na mpira mmoja, wakati timu yenye nidhamu Kilimani kutoka Mbinga ilipata fedha taslimu Sh. 200,000, mipira miwili na jezi seti moja.
Zawadi nyingine ilikwenda kwa kipa bora Ernest Kowero timu ya Mapera (B), aliyezawadiwa mpira mmjoja na fedha taslimu sh.100,000, mfungaji bora wa michuanpo hiyo, Faustin Hyera timu ya Kata ya Mapera A aliyefunga mabao 7, aliondoka na fedha taslimu sh.100,000 na mpira mmoja, wakati mwamuzi bora Germanus Mwambela, aliondoka na mpira mmoja na fedha taslimu Sh.100,000 na mashabiki wenye hamasa ni Kata ya Maguu (B), waliopata sh.100,000.
Mwandaaji wa mashindano hayo, Kinunda, alisema anafanya hivyo ili kurudisha fadhila kwa jamii, huku akiahidi kuyaboresha zaidi msimu ujao.
"Tunatakiwa kurudisha fadhila kule tulikotoka, ninawaahidi wananchi wa kata zetu, mwaka ujao tutayaboresha zaidi ili yawe na hadhi kubwa, ikiwezekana tuangalie jinsi ya kuunda timu ya kombaini," alisema Kinunda.
Mashindano hayo yalifunguliwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Joseph Mdaka na kufungwa na Karim Mzee kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo, yalianzishwa rasmi mwaka 2014 ambapo hadi sasa yametimiza miaka tisa.


No comments