Header Ads

ad

Breaking News

Watoto 24 wafanyiwa upasuaji wa moyo kambi ya matibabu JKCI

Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa

Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na mwenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia Mohammed Shihata kumfanyia upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu mtoto ambaye mishipa yake ya damu haipo katika mpangilio wake wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto inayoendelea JKCI.

Na Stella Gama, Dar es Salaam

WATOTO 24 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya ugonjwa huo inayoendelea katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Kambi hiyo ya upasuaji inafanywa na wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na wenzao wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha nchini Saudi Arabia.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mkuu wa kitengo cha upasuaji wa moyo kwa watoto wa JKCI, Dkt. Godwin Sharau, amesema licha ya kufanya kambi hiyo ya matibabu wamepata fursa ya kujifunza mbinu mpya za kitabibu na kuongeza ufanisi wa namna ya kufanya kazi kwa haraka katika muda mfupi hivyo, kuweza kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi.

 “Leo ni siku ya nne tangu kambi hii kuanza, tumefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto 24 na tunategemea hadi siku ya mwisho Alhamisi  tutakuwa tumefanya  upasuaji kwa watoto zaidi ya 30,” amesema Dkt. Sharau.

Dkt.Sharau ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto, amesema baadhi ya watoto ambao wamefanyiwa upasuaji ni wale waliozaliwa na matundu katika moyo, watoto ambao valvu zao hazijajitengeneza vizuri na wengine mishipa yao ya damu haijakaa katika mpangilio wake.

“Baada ya kuwafanyia upasuaji huu, watoto wengi wataweza kupona kabisa na kuendelea na maisha kama watoto wengine, lakini kuna wachache ambao upasuaji huu ni hatua katika hatua kadhaa za upasuaji ambazo zinahitajika ili waweze kupona,” amesema Dkt. Sharau.

Kituo hicho cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kimetoa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 520 ambavyo vinatumika katika upasuaji huo wa watoto.

Akizungumza kuhusu vifaa hivyo, Dkt.Sharau, ameshukuru kwa msaada huo na kusema kwamba,  vimesaidia watoto wengi kufanyiwa upasuaji kwani vipo vya kutosha.

“Wenzetu hawa kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha nchini Saudi Arabia wamekuwa wakija hapa nchini mara kwa mara na kutoa huduma ya  matibabu ya moyo kwa watoto na kusaidia vifaa vya matibabu hayo,” amesema Dkt.Sharau.

Kwa upande wake daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu, Abdulrahman Redhyan amesema kambi hiyo imekuwa ikidhaminiwa na Mfalme Salman wa nchini Saudi Arabia kuwawezesha watoto kupata matibabu na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa afya wa JKCI.

Dkt.Abdulrahman amesema jumla ya timu ya watu 26 kutoka nchini Saud Arabia ambao ni wataalamu wa usingizi, waendesha mashine za moyo, wauguzi na madaktari wameshiriki katika kambi hii, ili kuhakikisha watoto wengi wanafanyiwa upasuaji wa moyo kwa kipindi cha muda mfupi.

“Tunaamini kuwa, kuna watoto wengi wenye uhitaji wa huduma hizi za upasuaji wa moyo, ndiyo maana tumekuwa tukija kwa wingi ili kwa pamoja tuweze kuwasaidia watoto wetu kupata matibabu kwa haraka na kuwapunguzia maumivu ya ugonjwa,”amesema Dkt. Abdulrahman.

Naye, mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo, Mwamini Sabimana Rebeka kutoka nchini Congo, amesema mtoto wake amekuwa akisumbuliwa na magonjwa ya moyo tangu alipomzaa na kumpeleka katika hospitali mbalimbali bila ya mafanikio.

“Sikugundua mapema kama mtoto wangu alikuwa na shida ya moyo, hadi mwaka huu akiwa na miaka nane ndipo iligundulika kuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa nalo,” amesema Mwamini.

Mwamini amesema mtoto wake alikuwa na dalili mbalimbali ikiwemo kushindwa kupumua vizuri, kupata homa za mara kwa mara, kuwa mdhoofu, kuvimba mwili, lakini dalili zote hizo hospitali alizokwenda zilishindwa kutambua tatizo alilokuwa nalo. 

“Baada ya kukosa matibabu nyumbani Congo, nilikwenda Rwanda na baadaye kupata taarifa za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), nikafika hapa na kupatiwa matibabu kwa wakati.”

“Namshukuru Mungu mara baada ya mtoto wangu kupatiwa matibabu, anaendelea vizuri, si kama mwanzo, nawashukuru wataalamu wa afya wa JKCI kwa huduma zao nzuri sana, wananchi wenzangu kutoka Congo nawashauri mtakapopata matatizo ya moyo mfike hapa JKCI kwani, huduma za matibabu zipo na nzuri,” amesema Mwamini

Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na mwenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia Mohammed Shihata kumfanyia upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu mtoto ambaye mishipa yake ya damu haipo katika mpangilio wake wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto inayoendelea JKCI.
Mtaalamu wa kuendesha mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung Machine) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Robert Luchemba na mwenzake kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia wakiendesha mashine hiyo wakati wa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanyika JKCI.
Daktari bingwa wa usingizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Steven Nandi akiweka sawa mashine ya kuangalia mapigo ya moyo ya mgonjwa (monitor), wakati wa kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia.Picha zote na JKCI

No comments