WAZIRI MBARAWA ASEMA FIDIA ZITALIPWA KWA WANAOSTAHILI KISHERIA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akipokea taarifa kutoka kwa
Mkandarasi wa Kampuni ya CHICO (katikati), anayejenga barabara ya
Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojegwa kwa kiwango cha lami ambao ujenzi wake
umefikia takribani asilimia 77.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya
Mwigumbi, wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa KM
50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Shinyanga.

Meneja wa Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya (kushoto), akitoa
taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa (kulia), kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya
Usagara-Kisesa KM 16.135 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani humo

Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.135 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Mwanza.
…………………………………………………………………
Serikali imesema itawalipa fidia
kwa mujibu wa sheria wananchi wote waliopisha ujenzi wa barabara katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa wakati akizungumza na wananchi wa Mwigumbi mkoani
Shinyanga alipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi – Maswa yenye urefu
wa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa Kampuni ya
Chico na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambao unagharimu kiasi cha
Shilingi Bilioni 61.“Kila anayestahili kulipwa fidia atalipwa kama sheria inavyoelekeza na endapo akatokea yeyote mwenye malalamiko Serikali ipo itamsikiliza”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na Viongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mkoa ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na spidi inayotakiwa.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa
amewahimiza makandarasi wote nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa
wakazi wa maeneo husika inapopita miradi ya maendeleo ya ujenzi wa
miundombinu mbalimbali ili kuwapatia kipato na kuinua uchumi wao.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Shinyanga Eng.
Batholomeo Ndirimbi, amesema mpaka sasa tayari fedha zimetengwa kwa
ajili ya ulipaji fidia na watahakikisha kuwa fedha hizo zinalipwa kwa
watu sahihi wanaostahili fidia hizo.“Tutasimamia zoezi hili kwa umakini na kutoa fidia kwa wale wote wanaostahili kisheria”, amesema Eng. Ndirimbi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefikiwa asilimia 77 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua mradi
wa ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.1 inayojengwa kwa kiwango
cha lami ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na daraja la Nyashishi
lenye urefu wa mita 67.9 ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia
99.5 mkoani Mwanza.Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya, amesema ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vizuri na mkandarasi atamaliza kwa wakati uliopangwa na viwango walivyokubaliana katika mkataba.
No comments