MAKAMU AZINDUA TTCL PESA JIJINI DA ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia
Suluhu Hassan(kulia), akisikiliza maelezo kuhusu huduma mpya ya TTCL PESA kutoka kwa
Afisa
Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndugu Wazir W. Kindamba.. (PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

NA
OMR, DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan leo amezindua huduma mpya ya fedha mtandao ijulikanayo kama TTCL
PESA ya Kampuni ya Simu Tanzania TTCL. Uzinduzi huo umefanyika katika Makao
Makuu ya TTCL barabara ya Samora jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
Mheshimiwa Omari Nundu ambaye ni Mwenyeketi wa Bodi ya TTCL, Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Ujezi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Anjelina Madete, Afisa
Mtendaji Mkuu wa TTCL Bwana Waziri Kindamba, Wajumbe wa Bodi na
wafanyakazi wa TTCL.
Akizungumza katika hafla hiyo Makamu
wa Rais alisema uzinduzi wa huduma ya TTCL PESA ni mwendelezo wa jitihada za
Kampuni hiyo kurejea katika nafasi yake ya awali ya kuwa suluhisho la kweli la
utoaji huduma za Mawasiliano hapa nchini.
“Kuzinduliwa kwa huduma hii ni
uthibitisho mwingine kwamba, TTCL inatekeleza kikamilifu maagizo ya Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Rais wetu mpendwa Dkt John Pombe Magufuli ambaye
ameelekeza kuwa, Mashirika yote ya Umma yajiendeshe kwa faida, yatoe
gawio Serikalini, yawahudumie wananchi kwa kiwango cha juu kabisa cha
ubora na kwa gharama nafuu” alisema Makamu wa Rais.
Aidha, Makamu wa Rais alisisitiza
kwamba TTCL PESA itawezesha wananchi kutuma na kutoa pesa kwa viwango vya chini
kabisa kupita mitandao yote, pia itawezesha wananchi kulipia Bill za Umeme
(LUKU), Maji, Ving’amuzi na kuwezesha wateja kununua muda wa maongezi na
vifurushi vya data vya TTCL. Aliwataka TTCL kuendelea kuwa wabunifu
zaidi ili waweze kuongeza huduma nyingine kadiri mahitaji na siku
zinavyokwenda.
Akijibu kuhusu changamoto
zilizotajwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Makamu wa Rais alisema Serikali
inazijua na itaendelea kuzipatia majawabu. Hatahivyo aliwataka watumie vyema
rasilimali walizopewa ikiwamo Mkongo wa Taifa na Kituo cha Kuhifadhia
Kumbukumbu za kimtandao kupata pesa za kujiendeshea.
Makamu wa Rais pia aliipongeza menejimenti
ya TTCL kwa wazo lao la kufikiria kuanzisha kiwanda cha simu hapa nchini.
Alisema “msisitizo wa serikali yetu kwa sasa ni ujenzi wa uchumi wa kipato cha
kati ifikapo 2025 kupitia uwekezaji katika viwanda hivyo wazo lenu la ujenzi wa
kiwanda cha simu limekuja wakati muafaka”.
Mwisho, Makamu wa Rais alisema TTCL PESA itatoa fursa kubwa
ya ajira kwa wananchi kuwa mawakala na itarahisisha shughuli za kiuchumi
hasa biashara na hivyo aliwasihi wananchi kuonesha uzalendo wao kwa kutumia
huduma za TTCL.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndugu Wazir W. Kindamba (kulia)
akimuonesha namna ya kutumia huduma ya TTCL Pesa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kukamilika kwa
uzinduzi wa TTCL Pesa uliofanyika Makamo Makuu ya TTCL barabara ya Samora
jijini Dar Es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndugu Wazir W. Kindamba
(katikati) pamoja na Mwenyekiti ya Bodi ya TTCL Mhe. Omari Nundu wakimuonesha
kwa vitendo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan jinsi pesa inavyotumwa na kupokelewa kupitia huduma ya TTCL Pesa
mara baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa TTCL Pesa uliofanyika Makamo Makuu ya
TTCL barabara ya Samora jijini Dar Es Salaam.
No comments