WAAMUZI WA DJIBOUTI KUCHEZESHA TAIFA STARS DHIDI YA LESOTHO
![]() |
Nahodha wa timu ya Taifa Stars, Mbwana Samatta |
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF), limetangaza wamuzi wa mchezo kati ya Tanzania na Lesotho
unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Juni 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam
ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa CAF, waamuzi hao ni
Abdillah Mahamoud – atakayekuwa mwamuzi wa kati wakati wasaidizi wake ni
Gamaladen Abdi na Farhan Bogoreth wakati mwamuzi wa akiba atakuwa
Twagirumukiza Abdoulkarim kutoka Rwanda huku Kamishna akiwa ni Amir
Hassan wa Somalia
Waamuzi hao pamoja na kamishna
wanatarajiwa kufika Dar es Salaam, Tanzania kesho Ijumaa kwa ndege ya
Shirika la Ndege la Kenya (KQ) wakati wapinzani wa Taifa Stars wanaingia
jioni ya saa 11.55 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini. Timu
hiyo itafikia Hoteli ya Southern Sun, Dar es Salaam.
Mchezo kati ya Taifa Stars na
Lesotho, utafanyika kuanzia saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam uliko
Chamazi, Dar es Salaam na ili kuwapa fursa Watanzania wengi kushuhudia
mchezo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeondoka
kiingilio cha Sh 15,000.
Hivyo sasa Viingilio katika mchezo huo vitakuwa ni Sh 10,000 kwa Jukwaa Kuu wakati mzunguko itakuwa ni Sh 5,000.
Kujiandaa na Mchezo huo Taifa
Stars ilipiga kambi hapa nchini kuanzia Mei 23, mwaka huu kabla ya
kwenda Alexandria, Kaskazini kabisa mwa nchi ya Misri ambako ilipiga
kambi ya wiki. Kambi hiyo ilifurahiwa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars,
Salum Mayanga.
Mchezo huo dhidi ya Lesotho
utakuwa ni wa kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi
muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za
mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.
Mbali ya Lesotho na Tanzania,
mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia
wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza
pia kuwania nafasi hiyo.
No comments