“VIJANA WA PUGU 1,218 NA NEEMA YA AJIRA ZA JPM RELI YA STANDARD GAUGE”

Na Judith Mhina – MAELEZO
Kufuatia agizo la Rais John Pombe
Magufuli la kumtaka Mkandarasi atakayesimamia ujenzi wa Reli ya Standard
Gauge kutoa kipaumbe cha ajira kwa vijana wa Kata ya Pugu, wilayani
Ilala, tayari maombi ya Vijana 1,218 yamewasilishwa.
Wakielezea wakati wa mahojiano na
Idara ya Habari (MAELEZO) ofisini kwao leo kuhusu utekelezaji wa agizo
la Rais juu ya ushiriki wa vijana katika shuhguli mbalimbali za ujenzi
wa reli hiyo, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Kata za Pugu Bombani
na Pugu Stesheni wamesema kati ya idadi hiyo, Wanaume ni 945 na
Wanawake 273.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa
Pugu Stesheni Bwana Sifa Makakala amesema katika Kata yake yenye wakazi
7,636 jumla ya vijana wa kike 396 na vijana wa kiume 88 wameomba kufanya
kazi katika ujenzi wa Reli ya Stardard Gauge. Aidha, Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Kinyamwezi Bwana Mkumbo David amesema, katika Kata
yake yenye wakazi 7,573 jumla ya vijana wa kike 25 na wa kiume 35
wameomba ajira.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa wa “Kwa Mustafa” Bibi Bahati Usinzi amebainisha kuwa, katika Kata
yake yenye Wakazi 9,705 wakiwemo wanawake 5,593 na wanaume ni 4,412,
jumla ya vijana wa kiume 214 na wa kike 60 wameomba ajira.
Akihitimisha taarifa ya
utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, Mwenyekiti wa Mtaa wa Pugu
Bombani, Bwana Gido Lupiana amesema, “Vijana wengi wamepitisha barua zao
za maombi ya ajira katika mtaa wangu, lakini kwa bahati mbaya sina
kumbukumbu sahihi.” Hata hivyo, kwa makisio amesema jumla ya vijana 100
wameomba kupitia Mtaa wa Bombani na wengine 300 waliotoka nje ya Mtaa
huo na mikoani.
Kwa mujibu Kaimu Mtenda Mkuu wa
Kampuni Hodhi wa Mali za reli-RAHCO Bwana Masanja Kadogosi, takriban
Wafanyakazi 154 wameajiriwa katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Standard
Gauge katika vituo vya maandalizi vya Soga na Ngerengere ambapo Mkataba
wa ujenzi wa reli hiyo umetamka kuwa ajira za kiufundi asilimia 80
watatoka Uturuki na asilimia 20 Watanzania.
Aidha, kwa upande wa nguvu kazi
na zile za mtambuka, asilimia 80 ya waajiriwa wanatakiwa wawe Wazawa na
Asilimia 20 Wageni. Mradi wa reli ya standard gauge una jumla ya nafasi
za ajira 6,000 za watanzania.
Kadogosi ametoa wito kwa Wananchi
kuwa makini na watu wanaodai kuwa wameingia Mkataba na RAHCO kama wakala
wa kuwatafutia watu kazi katika ujenzi wa Reli hyo. “Tumesikia kuna
watu wanachukua fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi ya kupatiwa kazi
RAHCO.” Alisisitiza Bw. Kadogosi.
“Tupo kwenye maandalizi ya
kufungua mtandao wa RAHCO, mara utakaofunguliwa tutaweka nafasi zote za
kazi pamoja na zile za ukandarasi. Pia RAHCO itaandaa chapisho maalum
kwa Wakandarasi wazawa kuwaelezea fursa zinazopatikana ili waweze
kuzichangamkia kama alivyosisitiza Rais Magufuli,”Amesema Kadogosi.
Akiwa katika uzinduzi wa ujenzi wa
Reli ya Standard Gauge tarehe 12 Aprili mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa agizo kuwa, vijana
wa Kata ya Pugu Bombani na Pugu Stesheni wapewe upendeleo maalum katika
ajira zitakazotolewa na Kampuni ya Ujenzi ya YAPI kutoka Uturuki.
No comments