TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA KUTOKWA DAMU MKOANI KIGOMA

Utangulizi
Ugonjwa
wa Ebola umeendelea kuenea katika nchi za Afrika ya Magharibi ambapo
hadi sasa nchi tatu ambazo ni Guinea, Liberia na Siera Leone,
zimeendelea kutoa taarifa za wagonjwa wapya. Aidha, mpaka tarehe 19
Julai 2015, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni
27,705 na vifo 11,269. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imejiandaa
vyema kudhibiti ugonjwa huu iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na
kutengeneza mpango kazi wa udhibiti wa ugonjwa huu wa miaka mitatu
kuanzia 2015 hadi 2017.
Historia ya Mgonjwa
Mnamo
tarehe 9 Agosti 2015, mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika
kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa
Kigoma Maweni akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za
mwili hasusan kwenye fizi, macho na masikio. Vile vile alikuwa na dalili
za kuchoka na mwili kuwasha. Mgonjwa huyu hakuwa na homa. Alipata
matibabu katika hospital hiyo na kwa bahati mbaya mnamo tarehe 10
Agosti, 2015 mgonjwa huyu alifariki dunia. Mgonjwa huyu alikuwa hana
historia ya kusafiri kutoka nje ya mkoa wa Kigoma wala kutembelewa na
mtu aliyesafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zenye ugonjwa wa Ebola.
Mgonjwa
huyu alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi
katika kambi ya Nyarugusu kwa miaka mitatu. Mgonjwa huyu alikuwa
mmojawapo wa wakimbizi waliokuwa wasafirishwe katika mpango wa kawaida
chini ya Shirika la Kimataifa linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani.
Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9 Agosti 2015.
Hatua zilizochukuliwa
- Mgonjwa huyu alipatiwa matibabu katika hospitali ya Maweni Kigoma mpaka mauti ulipomkuta.
- Uongozi wa Afya Kigoma unafuatilia ndugu wa karibu wa mgonjwa huyu, pamoja na wahudumu wa Afya waliomuhudumia mgonjwa huyu kuona kama wataonyesha dalili zinazofanana na ugonjwa aliokuwa nao mgonjwa huyu. Ufuatiliaji huo umeanza tarehe 9 Agosti 2015. Mpaka leo hakuna mtu mwingine, aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu.
- Sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha ugonjwa huu.
- Mazishi ya marehemu huyo yamefanyika chini ya uangalizi wa Afya mkoa, kwa kuzingatia Utaratibu wa Kanuni za Kimataifa za kuzuia maambukizi.
Hitimisho
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa mpaka
sasa, hakuna uthibitisho wowote kuwa mgonjwa huyu amekufa na ugonjwa wa
Ebola. Aidha kwa kuwa ugonjwa bado unaendelea nchi za Afrika Magharibi,
Wizara inazidi kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na
ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza. Ikiwa ni pamoja na
- Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
- Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutoa huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa kifo kitatokea.
- Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
- Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
- Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
- Kunawa mikono mara kwa mara ili kuepuka kusambaza ugonjwa ikiwa mtu atakuwa ameshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
- Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itatoa taarifa pindi majibu ya maabara yatakapopatikana.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali – Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
12 Agosti, 2015
No comments