Header Ads

ad

Breaking News

Yanga yaikaribi Simba, Coastal waipiga Mtibwa Sugar 3-1


Yanga wakishangilia


 
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, wamezidi kumsogelea mtani wao wa jadi, Simba, baada ya kuilaza Ruvu Shooting mabao 3-2, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga walianza mchezo taratibu na kujikuta wakipigwa bao la kwanza dakika ya tatu likifungwa na Abraham Mussa, aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Michael Aidan.

Bao hilo liliwaongezea nguvu Ruvu Shooting na kuwawezesha kupata bao la pili dakika ya 10 lililofungwa na Seif Abdallah, baada ya mabeki wa Yanga wakifikiria kuwa ameotea.

Yanga walijibu mashambulizi ambapo dakika ya 16, Mbuyu Twite, aliifungia timu yake bao la kwanza kwa shuti kali la mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.


Mashambulizi ya Yanga yalizaa matunda dakika ya 20, baada ya Jerryson Tegete, alipata nafasi nzuri ya kufunga bao, lakini alishikwa na kigugumizi cha miguu na mpira ukaokolewa na mabeki wa Ruvu.

Dakika ya 36, Tegete  alifanikiwa kuipatia timu yake bao la pili, baada ya kumfunga kipa Benjamini Haule wa Ruvu Shooting, ambaye alikuwa na kazi kubwa ya kuokoa mashuti ya wapinzani wao.

Dakika ya 57, Ruvu Shooting walifanya shambulizi la nguvu kupitia kwa Ibrahim Shaaban, lakini tayari mwamuzi Mohamed Mkono kibendera chake kilikuwa juu kuashiria kuwa aliotea.

Didier Kavumbagu, aliifungia Yanga bao la tatu, baada ya kuichambua ngome ya wapinzani wao na kuutumbukiza mpira wavuni.

Wakicheza kwa kujiamini na kuliandama lango la wapinzani wao, Twite alipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 83, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango la Ruvu Shooting.
Hata hivyo, Ruvu itabidi wajilaumu wenyewe baada ya kushindwa kuitumia vizuri nafasi waliyopata kusawazisha bao dakika ya 85, wakiwa wamewazidi ujanja mabeki wa Yanga, na kukosa bao.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 14, ikiwa katika nafasi ya tatu, ikitanguliwa na Simba yenye pointi 17, na Azam FC yenye pointi 16.


Kutoka Mkwakwani Tanga, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa, Coastal Union jana iliibuka na ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Mtibwa Sugar. Mabao ya Coastal yalifungwa na Juma Jabu, Daniel Lyanga na Lameck Dayton, wakati bao la Mtibwa lilifungwa na Salum Sued.
 


Yanga: Yaw Berko, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Rashid Gumbo, Haruna Niyonzima, Jerrson Tegete, Didier Kavumbagu, David Luhende.

Ruvu Shooting: Benjamin Haule, Michael Aidan, Baraka Jafar, George Otei, Ibrahim Shaaban, Ernest Ernest, Raphael Kyala, Hassan Dilunga, Seif Abdallah, Abrahaman Mussa, Said Dilunga.

No comments