SuperSport kuonesha mechi 5 live
Sunday Kayuni (kulia), akiwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga |
KITUO cha Televisheni cha SuperSport
kinatarajiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi tano za Ligi Kuu Bara,
itakayoanza kutimua vumbi Septemba 15, mwaka huu.
Akizitaja mechi hizo zitakazorushwa moja
kwa moja jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa, hatua hiyo ya kurusha matangazo ya mechi
hizo kupitia chaneli ya SuperSport, imefikiwa baada ya kutaka kuwa mmoja wa
wadhamini wa michuano hiyo kwa msimu ujao wa mwaka 2013/2014.
Wambura alisema kuwa, mechi zilizopewa
jina la Super Weekend ni mechi kati ya Azam FC na JKT Ruvu itakayochezwa katika
Uwanja wa Chamanzi, Septemba 28, Simba na Tanzania Prison itakayochezwa katika Uwanja
wa Taifa, Septemba 29 na Yanga dhidi ya African Lyon itakayochezwa Septemba 30 Uwanja
wa Taifa.
Alisema kuwa, mechi nyingine ni kati ya
Ruvu JKT na Mtibwa Sugar, itakayochezwa
Oktoba Mosi na mechi kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Oktoba 3, kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Wambura alisema kuwa,
suala la Hati za Uhamisho (ITC), kwa wachezaji Pascal Ochieng na Salum Kinje,
wote wa klabu ya Simba, zimewasili.
“ITC zao zimefika, wamekamilishiwa, tayari
kwa kucheza katika michuano ya Ligi Kuu Bara, lakini mchezaji wa Mtibwa Sugar, Hassan
Isiko, kutoka Bull FC ya Uganda, bado ITC yake haijafika,” alisema
Alipoulizwa kuhusu sheria inasemaje juu ya
mchezaji huyo, Wambura, alisema kuwa, sheria za Shirikisho la Soka Duniani
(FIFA), litamruhusu mchezaji huyo kuchezea katika klabu hiyo kwa miezi mitatu, kama
tu klabu hiyo iliomba ITC katika muda uliotakiwa na kucheleweshwa na klabu yake
ya zamani.
No comments