Simba wawawekea pingamizi Yondani, Twite TFF
![]() |
Kelvin Yondani |
KLABU ya Simba imeweka pingamizi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), la wachezaji wa Yanga, Kelvin Yondani na Mbuyi Twite, ambao wamesajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Awali, mabingwa hao wa soka nchini, Simba, walidai
kuwa, Yondani bado ni mchezaji wao, kwani ana mkataba nao, huku wakidai Twite,
ambaye amesajiliwa na Yanga akitokea APR ya Rwanda, ni mchezaji wao pia.
Simba walimsajili Twite siku chache, baada ya
kumalizika kwa michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambapo kwa upande
wa beki wake wa zamani Yondani, aliamua kutimkia Yanga, licha ya kuwa na
mkataba na Simba wa mwaka mmoja.
Akithibitisha taarifa hizo, Ofisa wa Habari wa
Simba, Ezekiel Kamwaga, alikiri kupeleka pingamizi hilo, baada ya pazia la
usajili wa ligi kuu kwa wachezaji wa ndani kufungwa.
“Kweli tumepeleka pingamizi TFF kuwapinga wasichezee
Yanga, kutokana Simba kuwa na mikataba nao,” alisema Kamwaga.
Kwa upande mwingine, Kamwaga alisema uongozi wa
Simba umewasilisha pingamizi lingine la kutokuwa na imani na Kamati ya Katiba
Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji.
Kamwaga alisema Simba imefikia hatua hiyo ya
kuipinga kamati hiyo iliyo chini ya Alex Mgongolwa, kutosikiliza pingamizi hilo
kutokana na wajumbe wake kuwa na mapenzi na Yanga.
Kiongozi huyo wa Simba alisema kabla ya kamati hiyo
kusikiliza shauri hilo, Mgongolwa alisikika akusema kuwa, katika mkataba wa
Simba na Yondani, una mapungufu.
Kamwaga alisema kauli ya mwenyekiti huyo imewapa
hofu na hivyo kutokuwa na imani katika kusikiliza pingamizi hilo.
Wajumbe wengine waliowekewa pingamizi kutosikiliza
shauri la Yondani na Twite ni Imani Madega, Lloyd Nchunga na Omary Gumbo.
Akitaja sababu za kuwawekea pingamizi ni kutokana na
kuonesha mapenzi yao juu ya klabu ya Yanga.
Ofisa habari huyo wa Simba alisema moja ya njia
ambazo wanatumia wajumbe hao katika kamati hiyo, ni kupiga kura na kitendo cha
wajumbe wa kamati hiyo kuwa na mapenzi na Yanga kina lenga kutowatendea haki
mabingwa hao wa ligi kuu.
Kamati hiyo ya Mgongolwa inaundwa na wajumbe saba,
ambapo mapendekezo hutolewa kwa idadi ya wajumbe kufikia nusu yao kujumlisha
mmoja.
Super Star lilimtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Angetile
Osiah, ili kuthibitisha juu ya taarifa hizo za pingamizi, alisema ofisi yake
imepokea pingamizi moja ya Simba juu ya Yondani na Twite, kwa upande wa wajumbe
Kamati ya Utendaji alidai hajapokea.
“Nimepokea pingamizi la Simba juu ya Yondani na
Twite, na si vinginevyo,” alisema Osiah.
Kwa upande mwingine, Osiah alishindwa kulitolea
ufafanuzi pingamizi la Simba kwa Twite kutokana na timu hiyo kutowasilisha jina
lake katika fomu za usajili, hivyo kudai suala hilo litasikilizwa na Kamati ya
Katiba.
No comments