Header Ads

ad

Breaking News

MSAMA PROMOTION YASAIDIA MATIBABU YA MCHEZAJI WA ZAMANI WA TAIFA STARS


  Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari.
 Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama (kushoto) akimkabidhi msaada wa fedha taslimu sh. milioni moja  mchezaji wa zamani wa Simba, Mtibwa na Taifa Stars, Alphonce Modest kwa ajili ya kumsaidia katika matibabu ya ugonjwa wa mifupa unaosababisha miguu kufa ganzi ‘yabisi baridi’. Modest nasumbuliwa na ugonjwa huo tangu mwaka 2011. Kwa yeyote anayeguswa na tatizo lake awasiliane na mtangazaji wa Chanel 10, Said Kilumanga (wa pili kulia) kwa kupitia namba 0718 427426. Wa Pili kushoto ni Mhariri Kiongozi wa Champion, Saleh Ally.
 Mtangazaji wa Chanel 10, Said Kilumanga  akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa rai kwa watu mbalimbali kujitolkeza katika kumsaidia mchezaji wa zamani wa Simba na timu ya Taifa Alfonce Modest ambaye anasumbuliwa na matatizo ya miguu.
Beki wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Alfonce Modest akimshukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions baada ya kumsaidia kiasi cha sh milioni moja kwa ajili ya kuanza matibabu ya miguu.
Mhariri Kiongozi wa Champion, Saleh Ally akizungumza na waandishi wa habari kuhusu watu mbalimbali kujitokeza katika kusaidia matibabu ya mchezaji wa zamani wa timu ya Simba na Taifa Stars, Alfonce Modest.


DAR ES SALAAM, Tanzania
 MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama,  ametoa msaada wa sh milioni moja kwa nyota wa zamani wa soka, Alfonce Modest.
Modest aliyewahi kuwika na timu za Pamba ya Mwanza, Simba, Mlandege na Taifa Stars, anasumbuliwa na matatizo ya miguu kukosa nguvu.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada wake kwa Modest kwenye Ofisi za Kituo cha Televisheni ya Channel Ten, Msama alisema amefanya hivyo kutokana na kuguswa na tatizo hilo.
Alisema, akiwa mdau wa masuala ya kijamii, ameona atoe hicho kidogo kama mwanzo wa fedha za matibabu kwa mkongwe huyo.
“Mimi nimejitolea kumsaidia ndugu yangu Modest, nimemsaidia kama Mtanzania mwenzangu, aliyewahi kutoa mchango mkubwa katika soka ya nchi hii,” alisema Msama.
Msama ambaye ni mwasisi wa matamasha ya muziki wa Injili nchini, amewataka wengine wenye moyo kujitokeza kumsaidia Modest.
Akizungumza baada ya kupokea kiasi cha awali cha sh 600,000, alimshukuru Msama kwa moyo wa kusaidia wenye shida na matatizo mbalimbali kwenye jamii.
“Nimekuwa nikimsikia tu Msama, kumbe ndiyo huyu, namshukuru sana, naamini sasa nitapata matibabu ya uhakika,” alisema Modest.
Aidha, alitoa shukrani kwa wote waliofanikisha suala hilo akiwamo Said Kilumanga na Saleh Ally.
Akizungumza baada ya Modest kukabidhiwa msaada huo, Kilumanga alisema Modest ataanza kupatiwa vipimo kesho kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo la mifupa.
Alitoa wito kwa  atakayeguswa na tatizo la Modest afike ofisi za Channel Ten kwa ajili ya kukutanishwa na mhusika.
Akielezea kwa undani kuhusu tatizo lake, Modest alisema, matatizo ya afya yake yalianza mwaka 2010, wakati huo alikuwa akisumbuliwa na mapafu kujaa maji.
Alisema, baada ya kulazwa kwa miezi mitatu katika Hospitali ya Lugalo, alipata nafuu kiasi, lakini mwaka uliofuata 2011, akaanza kuhisi viungo kukosa nguvu.
Alisema, licha ya kuhangaika huku na huko, tatizo hilo la ganzi kwenye viungo likazidi na kusababisha mwili wake kushindwa kuwasiliana.
“Ganzi ilianzia kwenye viungo vya miguu, lakini sasa imepanda hadi kwenye mikono na maeneo mengine ya mwili, kwa kweli naumwa, niombeeni kwa Mungu, niweze kupona,” alisema Alfonce aliyestaafu soka mwaka 2002, akiwa katika kikosi Mtibwa Sugar. www.francisdande.blogspot.com

No comments