UONGOZI TWIGA STARS WATOA TAMKO
Uongozi wa Twiga
Stars umekana kuwepo vitendo vyovyote vya kinyume na maadili kwa wachezaji wa
timu hiyo ambayo hivi karibuni ilitolewa kwenye mechi za mchujo za michuano ya
Afrika kwa Wanawake (AWC).
Wakizungumza na
waandishi wa habari leo (Julai 2 mwaka huu), Meneja wa Twiga Stars, Furaha
Francis na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa wamesema
hakuna vitendo vya aina hiyo.
Mkwasa amesema alikaririwa
vibaya kuhusu suala hilo wakati akiwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni
cha Star Tv kutokana na swali alilokuwa ameulizwa kuhusiana na vitendo hivyo.
“Ukifuatilia
mahojiano yangu na Star Tv mimi sikusema kuwa kuna vitendo hivyo. Tatizo nadhani
lilianzia kwa magazeti yaliyonukuu kupitia Star Tv, na wala kujiuzulu kwangu
hakukuhusiana na hilo, nimewajibika kama kocha kutokana na kutolewa na
Ethiopia,” amesema Mkwasa.
Naye Furaha Francis
amesisitiza kuwa hakuna vitu vya aina hiyo katika timu hiyo, na kama kuna mtu
ana ushahidi na hilo ni bora akauonesha badala ya kuzungumzia uvumi kuliko
ukweli.
“Ukweli ni kwamba si
sisi na wachezaji tu ambao hatukufurahishwa kutolewa na Ethiopia, wapo
Watanzania wengi ambao hawakufurahishwa na matokeo yale. Twiga Stars si timu ya
kudumu, haikai na wachezaji kwa muda wote, kila mchezaji ana timu yake.
“Madai yanayoenezwa
na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu vitendo hivyo yametuchafua sana. Tunaomba
kama kuna mtu ana ushahidi na hilo atueleze kuliko kuendelea kutuchafua,”
amesema.
No comments