RUVUMA YAIFANYIA MAUAJI LINDI 7-2
Timu ya Ruvuma
imethibitisha kuwa mwiba mkali katika michuano ya Copa Coca-Cola mwaka huu
baada ya leo asubuhi (Julai 2 mwaka huu) kuishushia Lindi kipigo cha mabao 7-2.
Hadi mapumziko kwenye
mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani, washindi ambao
kwa matokeo hayo wamejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza 16 bora walikuwa
mbele kwa mabao 3-0.
Waliotikisa nyavu ni
Anthony Christian dakika ya 23 na 50, Edward Songo dakika ya 27, 75 na 86 na
Sunday Leonard dakika ya 32 na 60. Mabao ya Lindi yalifungwa na Salum Mnyamwile
dakika ya 18 kwa njia ya penalti na lingine dakika ya 48 kupitia kwa Mwarami
Maundu.
Nayo Tanga imepata
ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kuifunga Manyara mabao 2-0
katika mechi ya kundi B iliyochezwa Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mabao ya
washindi yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 47 na Issa Mwanga dakika ya 60.
Katika mechi tatu
zilizotangulia Tanga ilitoka sare ya mabao 3-3 na Morogoro, ikapata sare
nyingine ya 1-1 dhidi ya Mwanza, na baadaye 1-1 na Tanga.
Kagera imeendelea
kujitutumua katika michuano hiyo baada ya kupata ushindi wake wa pili katika
kundi D kwa kuilaza Kusini Unguja bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa
Tanganyika Packers ulioko Kawe jijini Dar es Salaam.
Bao lake lilifungwa
dakika ya 76 na Novati Sebastian. Mechi iliyopita Kagera iliifunga Tabora mabao
2-0 baada ya kuteleza katika mechi mbili za kwanza kwa kufungwa na Kilimanjaro
na Singida.
Mechi nyingine
ilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo Kinondoni iliibuka
na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mara.
No comments