ASET yaandaa onesho maalum Jumapili
![]() |
Asha Baraka |
KAMPUNI ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET) inayomiliki bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', imeandaa onesho maalum la kuvitambulisha vipaji vipya Jumapili katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Asha Baraka, alisema onesho hilo limepewa jina la ASET Academia litakalowawezesha masbahiki wa muziki kuviona vipaji vinavyopikwa na bendi hiyo.
Asha alisema wanamuziki hao chipukizi walipatikana hivi karibuni baada ya kufanyika mchujo kuanzia waimbaji, wapiga vyombo na marapa.
Alisema kwa bendi itayovutiwa na chipukizi hao, italazimika kulipa kiasi cha sh. milioni tano ambazo ni gharama za mafunzo waliyopewa na kampuni hiyo.
Asha alisema vipaji hivyo vipya vilikuwa vikinolewa na Rais wa bendi ya FM Academia, Nyoshi El Sadat 'Sauti ya Simba' na Mkurugenzi wa bendi ya Bantu Group, Hamza Kalala.
"Lengo la kufanya hivi ni kusaka vijana wenye vipaji ambao wamejaa mitaani, lakini hawana mtu wa kuwaendeleza, tunaamini wameiva na wataonesha kile ambacho wamefundishwa," alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, lengo lao ni kuhakikisha wanawawezesha waimbaji chipukizi kuendeleza vipaji vyao kwa manufaa ya familia zao.
No comments