Darts kuanza kurindima Septemba 23
Meneja wa Bia ya Safari Lager Oscer Shelukindo (kushoto) na Mwenyekiti wa Mchezo wa Vishale (Darts) Tanzania, Gesase Waigama.
MASHINDANO ya vishale (darts), ya Taifa yatafanyika Septemba 23 hadi 25, mkoani Tanga.
kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, imejitosa kudhamini mashindano hayo, ambayo yatashirikisha mikoa mbalimbali nchini.
Meneja wa bia ya Safari Oscar Shelukindo, amesema wamedhamini mashindano hayo kwa sh. milioni 20.
Alisema mashindano hayo yanatarajia kushirikisha mikoa 15 ya Tanzania Bara na kwamba, lengo la TBL kudhamini mashindano hayo ni kutaka kuendeleza vipaji vya mchezo huo na kurudisha hadhi yake kama zamani.
Amesema watahakikisha wanaongeza bodi nyingi za kuchezea mchezo huo, ili waweze kupata wachezaji wengi zaidi.
Mwenyekiti wa Chama cha Vishale Tanzania (TADA), Gesase Waigama, amesema TBL kupitia bia yake ya Safari Lager, imekuwa mkombozi wao, hivyo wanaipongeza kwa juhudi zao za kuendeleza mchezo huo.
Mashindano hayo yatajulikana kwa jina la TADA Cup, yataihusisha mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Singida, Dodoma, Arusha, Kagera, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Manyara, Tabora, Musoma, Mtwara Shinyanga na Kigoma.
No comments