Header Ads

ad

Breaking News

Magonjwa ya moyo Asilimia 80 yanazuilika kwa kinga na uchunguzi wa mapema

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Peace Masaoe akimuelezea dalili za magonjwa ya moyo mwananchi aliyefika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani.


Na mwandishi maalumu, Dar es Salaam

ASILIMIA 80 ya magonjwa ya moyo yanayosababisha vifo yanaweza kuzuilika kwa kufanya uchunguzi wa afya mapema, kula chakula ambacho kinalinda afya ya moyo, kutoishi maisha bwete na kupata huduma za afya kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Samweli Rweyemamu wakati wa kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanyika katika Hospitali hiyo katika kuadhimisha siku ya moyo duniani.

Dkt. Rweyemamu alisema kupitia kambi hiyo kuna watu ambao hawakuwa wanajua kama wana tatizo la shinikizo la juu la damu baada ya kupima ndio wakagundulika kuwa na tatizo hilo.

Mteknolojia Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Ashura Salum akimpima sukari kwenye damu mwananchi aliyefika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani.

“Jamii inatakiwa kujikinga na magonjwa haya ya moyo yanayoweza kuepukika kwa kuwa na mtindo bora wa maisha, kuacha kutumia vilevi vinavyoweza kuathiri afya zao pamoja na kupata mlo kamili.”

“Asilimia kumi ya watu tuliowaona toka jana tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu hivyo kuwaanzishia kliniki katika Taasisi yetu ili kwa pamoja tuweze kufuatilia afya zao na kuwasaidia kutokupata madhara makubwa zaidi,” alisema Dkt. Rweyemamu

Dkt. Rweyemamu aliongeza kuwa JKCI imeadhimisha siku ya moyo duniani kwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wananchi bila gharama kama sehemu ya taasisi hiyo kurejesha katika jamii na kuwapa nafasi wananchi ambao wasingeweza kuchunguza afya zao kutokana na hali za kiuchumi walizonazo.

“Tunaiomba serikali iweke miundombinu rafiki ikiwemo kugharamia matibabu makubwa yakiwemo ya moyo kwani wapo wananchi leo wametoka maeneo ya mbali kuja kupata huduma kutokana na huduma hizi kutolewa bila gharama,”alisema Dkt. Rweyemamu

Kwa upande wake mfamasia kutoka kampuni ya dawa ya Hetero Pharm Limited, Joseph Justine, alisema kampuni hiyo imeweza kutoa dawa bila gharama kwa wananchi waliopata huduma katika kambi hiyo ili huduma walizozipata ziweze kukamilika.

Mfamasia kutoka kampuni ya dawa ya Hetero Labs Limited Joseph Justine akimpatia dawa mwananchi aliyefika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani.


“Hii ni moja ya njia muhimu kwetu kurudisha katika jamii hivyo ninawakaribisha wananchi wanaotamani kujua afya zao waweze kufika hapa kwani watapata huduma bila gharama na wale watakaoandikiwa dawa tutawapatia dawa zao hapa”, alisema Joseph.

Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Hassun Rashid aliipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kuona umuhimu wa kuwafikishia huduma wananchi bila gharama kwani wapo wengi ambao wanahitaji huduma hizo lakini kutokana na hali zao kiuchumi wanashindwa kupata huduma.

Hassun alisema kupitia kambi hiyo ameweza kupata elimu nzuri kuhusu magonjwa ya moyo ikiwemo ugonjwa wa shinikizo la damu na namna ya kuepukana na magonjwa hayo, hivyo atatumia vizuri elimu hiyo kujikinga asipate magonjwa hayo.

“Nimefurahi sana leo nimeweza kupima moyo wangu na nimekutwa salama, kupitia elimu niliyoipata hapa nitahakikisha najilinda nisipate magonjwa ya moyo na kuwafundisha familia yangu ili nao wasiyapate,” alisema Hassun.

Fundi Sanifu wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Eliza Shuma, akimfanyia kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo mwananchi aliyefika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani.

Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Rajabu Hamis, akiwagawia wananchi vipeperushi vinavyoelezea magonjwa ya moyo, ugonjwa wa shinikizo la damu na lishe bora wananchi waliofika katika Hospitali ya JKCI-Dar Group iliyopo TAZARA Wilaya ya Temeke kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani. Picha na JKCI

No comments