Header Ads

ad

Breaking News

Kiwango cha uagizaji mafuta nchini kimeongezeka-Mtendaji Mkuu PBPA

Mtendaji Mkuu wa wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Simon, akiwasilisha wasilisho lake kwa wahariri na waandishi wa habari

Na Mwandishi Wetu

WAKALA wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), imetaja mafanikio 10 yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo kiwango cha uagizaji mafuta kuongezeka.

 Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, amesema kuwa, moja  mafankio ni kuokoa Sh.bilioni 225.6, baada ya kufungwa mifumo ya kusimamia upokeaji wa mafuta.

Simon amezungumza hayo katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, amesema serikali kupitia Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na wadau, waliweka mazingira mazuri kwa kampuni za mafuta kupata fedha za kigeni kutoka katika Benki za Biashara.

Mtendaji Mkuu huyo ameyataja mafanikio mengine ya PBPA, ni pamoja na usajili wa kampuni za uagizaji mafuta ambazo kwenye mchakato wa uagizaji mafuta zimeongezeka kutoka kampuni 33 za mwaka 2021 hadi kufikia kampuni 73 kwa mwaka 2025, ambalo ni ongezeko la asilimia 121.

Amesema wakala umesajili wazabuni 24 katika mfumo wa BPS kwa kipindi cha miaka minne kutoka mwaka 2021 hadi mwaka 2025, pamoja na kiwango cha uagizaji mafuta nchini kupitia mfumo wa BPS kuongezeka kutoka wastani wa tani 5,805,193 za mwaka 2021 hadi tani 6,365,986 za mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 9.6.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akieleza jambo katika kikao kazi cha Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), wahariri na waandishi wa habariS

Ameongeza kuwa, hadi Desemba 2025, jumla ya tani 7,090,165  zitakuwa zimeagizwa ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 11.4 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka uliopita.

Simon amesema kwamba, katika kipindi cha miaka 4 zabuni za uletaji mafuta nchini zimeongezeka kutoka zabuni 109 za mwaka 2021 hadi zabuni 118, ifikapo Desemba 2025, ambalo ni ongezeko la asilimia 8.

Kuhusu mikataba, Mtendaji mkuu amesema kuwa, mikataba ya zabuni za uagizaji wa mafuta nchini imeongezeka kutoka wastani wa mikataba 109 mwaka 2021 hadi kufikia wastani wa mikataba 118 itakapofika Desemba 2025, huku akiweka wazi kuwa, kwa miaka minne mikataba 589 imetekelezwa kwa ufanisi.

"PBPA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  tumeendelea kupanga ratiba za meli za kuleta mafuta nchini ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya bandari zetu na kupunguza gharama za meli kusubiri," amesema Simon.

Amesema hatua hiyo imesaidia kuokoa kiasi cha Dola milioni 11.5 sawa na Sh.bilioni 29.95 kwa mwaka ambazo zilikuwa zikitumika, hatua hiyo imesaidia kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini ambazo awali zilikuwa zikitumika kulipia gharama husika.

Mtendaji Mkuu huyo ameongeza uwa, PBPA imeendelea kutunza taarifa za mafuta yanayoingia nchini kupitia mfumo wa BPS, ambapo kuanzia Julai 2024, inasimamia na kutunza taarifa za meli zote zilizo nje ya Mfumo wa BPS zinazoshusha mafuta nchini na hivyo kuwa na taarifa sahihi za mafuta yote yanayopokelewa nchini.

"Hali ya upatikanaji mafuta nchini imeendelea kuwa ya uhakika katika kipindi cha miaka minne iliyopita, PBPA tumewezeshwa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kidunia kama Uviko-19 na vita kati ya Urusi na Ukrain, Iran na Israel."

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akitoa neno la shukrani

Amesema katika kipindi chote nchi imekuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji wakati wote pamoja na kuhudumia nchi jirani.

"Serikali imefunga mifumo wa kusimamia upokeaji wa mafuta nchini ikiwemo flowmeters na SCADA, ambazo zimechangia kuongeza udhibiti wa udanyanyifu katika kiasi cha mafuta yanayopokelewa kwenye maghala ya kuhifadhia, hivyo kupunguza upotevu wa mafuta," amesema.

"Baada ya kufunga mifumo hiyo, tunaokoa wastani Sh.bilion 56.4 kila mwaka hivyo, kwa miaka minne serikali imeokoa jumla ya Shilingi  bilioni 225.6 zilizokuwa zikipotea kutokana na upotevu wa mafuta."

Kuhusu ajira, Mtendaji mkuu amesema kuwa, katika kipindi cha miaka minne watumishi wapya 68 wa kada mbalimbali waliajiriwa kwa lengo la kutekeleza majukumu ya kuratibu uagizaji wa mafuta nchini na kusimamizi wa mfumo wa BPS.

PBPA umeendelea kuboresha usimamizi wa mfumo wa BPS ili kuendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini wakati wote na kwa bei stahiki zinazoendana na mwenendo wa mabadiliko ya bei katika soko la dunia, kuongeza kiwango cha mafuta kupitia mfumo wa BPS kwa kuvutia nchi zinaz0tegemea bandari za Tanzania.

Aidha, Wakala utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya mafuta vikiwemo vyombo vya habari katika kuendelea kuimarisha  mfumo wa BPS kwa maslahi mapana ya taifa.

Afisa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Alex Malanga, akiendesha kikao kazi

Mtendaji mkuu amesema kuwa, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia, PBPA umeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. 

Majukumu hayo ni pamoja na kusimamia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS), kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini muda wote, kukusanya mahitaji ya mafuta na kutangaza zabuni kwa ajili ya kuleta mafuta nchini.

"Kusimamia mikataba ya uagizaji mafuta na kuhakikisha mafuta yaliyoagizwa yanafika nchini kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kulingana mikataba husika, kusimamia utekelezaji wa taratibu za uagizaji wa mafuta nchini, ambazo zinajumuisha usajili wa kampuni za Uagizaji Mafuta nchini (OMCs) na usajili wa wazabuni. 

Ameongeza kuwa, upokeaji wa mahitaji ya mafuta kutoka kwa OMCs, uchakataji wa mahitaji yaliyopokelewa, utangazaji na ufunguzi wa zabuni shindanishi za kimataifa, usimamizi wa utekelezaji wa mikataba, kupanga ratiba za meli zinazoleta shehena za mafuta nchini na kutunza taarifa za meli zilizoleta mafuta.

Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Nishati, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali, Sura ya 245. Uanzishwaji wake  ulitangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 423 la Septemba 25, 2015. PBPA ilianza rasmi utekelezaji wa majukumu yake Januari 2016.

Maafisa waliohudhuria kikao kazi wakisikiliza

Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini wasilisho kutoka kwa Mtendaji Mkuu PBPA, Erasto Simon



No comments