Inovate yaita wadau kuutumia uwanja wake
UONGOZI wa Shule ya Awali na Msingi ya Inovate iliyopo Kitongoji cha Kibwende Kata ya Mlandizi Kibaha Vijijini Pwani, inawakaribisha wanaoandaa ligi mbalimbali kuutumia uwanja uliopo shuleni hapo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa shule hiyo, George Ndaki, akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo, baada ya hafla fupi ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mithihani iliyoshirikisha shule tofauti.
Alisema kwamba shule hiyo iliyopo kilometa chache kutoka Barabara Kuu itokayo Mlandizi kuelekea Bagamoyo ina uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, sanjali na netiboli ambavyo vimeandaliwa kulingana na vigezo vinavyohitaji.
"Kama mnavyoviona viwanja vyetu vimekidhi vigezo vinavyohitajika kwa ajili ya michezo ya mpira wa miguu sanjali na netiboli, kutokana na uhalisia huo milango ipo wazi kwa wadau wanaoandaa michezo husika waje kuvitumia," alisema Ndaki.
Aliongeza kuwa "Ligi ya Samia Super Cup iliyomalizika hivi karibuni ngazi ya Jimbo, hatua ya awali iliyochezwa kwenye Kata ambapo kwa Mlandizi ilitimua vumbi katika uwanja huu unaomilikiwa na shule," alisema Mkurugenzi huyo.Akizungumzia ushiriki wa michezo kwa shule hiyo, Ndaki alisema kuwa mara kadhaa imekuwa ikienda kushindana na shule nyingine zilizopo ndani ya Jimbo la Kibaha Vijijini, huku akieleza kuwa kuna wakati mwingine inafanya vizuri.
"Pasipokukisahau Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya (KIBAFA), wanapoandaa ligi ngazi hiyo wasisite kuleta michezo hiyo katika uwanja wetu," alisemalizia Ndaki.
No comments