Dkt.Mafumiko ataja mafanikio Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kipindi cha Miaka Minne ya Uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejielekeza katika huduma za uchunguzi wa kimaabara, utoaji wa ushahidi wa kitaalam, usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani.
Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, ameyasema hayo wakati wa kikao kazi kilichofanyika Julai 10,2025 jijini Dar es Salaam, kilichowahusisha wahariri na waandishi wa vyombo vya habari mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ofisi na maabara, uimarishaji wa matumizi ya tehama katika utoaji na mafunzo kwa wadau, kuimarisha huduma za uchunguzi wa kimaabara na ufanisi katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa kimaabara.
Dkt. Mafumiko amesema kuwa, uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa sampuli pamoja na vielelezo umeongezeka kutoka sampuli 155,817 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi kufikia sampuli 188,362 kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 21.
"Katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2024/2025, kuanzia Julai hadi Mei 2025, sampuli 175,561 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 92 ya lengo la kuchunguza sampuli 191,420," amesema.
Mkemia mkuu amesema kuwa, ongezeko la sampuli zinazochunguzwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, linatokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi na wadau wa mamlaka na ubora wa huduma za uchunguzi zitolewazo na mamlaka.
Amesema hali hiyo imetokana na ushirikiano na taasisi za Serikali za udhibiti ikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulenya (DCEA) na Jeshi la Polisi.
Zingine ametaja ni Mamlaka ya Mapato (TRA), wadau wa afya zikiwemo hospitali, Taasisi ya Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wadau wengine wanaotumia huduma za Mamlaka ili kupata uhakika wa ubora wa bidhaa zao.
Amesema mchango wa utoaji wa matokeo ya uchunguzi wa sampuli kwa wakati, umekuwa mkubwa katika kusaidia katika mnyororo wa haki jinai na kuwezesha utoaji wa haki stahiki katika vyombo vya maamuzi kwa wahusika na kwa wakati.
"Masuala ya kijamii yamepatiwa ufumbuzi, ikiwemo kupata uhalali wa wazazi kwa watoto, utatuzi wa migororo inayohusu mirathi, utambuzi wa miili ya waathirika iliyoharibika vibaya kutokana na majanga mbalimbali ikiwemo ajali za majini, magari, kuangukiwa na majengo, moto, ndege na matibabu kwa wagonjwa wanahohitaji huduma ya kusafishwa figo.Ameongeza kuwa, Mamlaka pia imefanya uchunguzi wa sampuli za maji tiba yanayotumika kwa wagonjwa wanaohitaji kusafisha figo na kupandikizwa figo, kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara kubainisha uhusiano uliopo kati ya mtoaji na mpokeaji wa figo kabla ya upandikizaji kufanyika.
"Tumehusika katika utambuzi wa jinsi tawala kwa kufanya uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara na kutoa ushauri stahiki kwa madaktari bingwa kwa lengo la kutoa matibabu kwa wagonjwa wenye changamoto ya jinsi na utambuzi wa sumu kabla ya kifo kutokea, kwa kubainisha sumu kwa wagonjwa wanaodhaniwa kuvuta, kunywa au kula chakula chenye sumu, ili kupata tiba sahihi na kwa wakati.
"Pia tumefanya utambuzi wa sumu baada ya kifo kutokea, kwa kubainisha sumu iliyosababisha kifo kwa waathirika, usalama na ubora wa bidhaa za viwandani na chakula, dawa (dawa za kisasa na dawa asili), mazingira na usalama mahala pa kazi kwa lengo la kuhakikisha afya ya jamii na mazingira inalindwa.
Dkt. Mafumiko amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia imeiwezesha mamlaka hiyo kununua mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara.
Uwekezaji katika ununuzi wa mitambo ya uchunguzi wa kimaabara kwa mujibu wa Dkt. Mafumiko, umeongezeka kwa asilimia 23.6, kutoka uwekezaji wa Sh. bilioni 13.6 kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 hadi 2021/2022 na kufikia Sh. bilioni 17.8 kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kwa kuongeza mitambo mikubwa 16 na midogo 274.
Mkemia Mkuu ameongeza kuwa, ununuzi wa mitambo hiyo umeimarisha uchunguzi wa kimaabara na kuendelea kutoa huduma bora za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
"Mamlaka imefanikiwa kuendelea kutoa huduma za uchunguzi wa kimaabara na matokeo yake kukubalika katika ngazi na viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Mafanikio hayo yametokana na utekelezwaji wa mifumo miwili ya
ubora na umahiri ya kimataifa, yenye Ithibati ya Mifumo ya Usimamizi wa Ubora
(ISO 9001:2015) ya uendeshaji wa shughuli za mamlaka uliyohuishwa kwa mara nne
mfululizo na Mfumo wa Ithibati katika Umahiri wa Uchunguzi wa Kimaabara (ISO
17025:2027)," amesema Dkt. Mafumiko.
Amesema Mamlaka imefanikiwa kupata ithibati katika umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO 17025:2027) kwenye maabara zake sita, ambazo ni Maabara ya Vinasaba vya Binadamu, Mikrobiologia, Sayansi Jinai Toksikologia, Mazingira na Kanda ya Ziwa, Mwanza ikiwemo Maabara ya Chakula.
Dkt. Mafumiko amesema mafanikio hayo ni muhimu kwa kuwa, kunaifanya Mamlaka kukidhi matakwa ya kisheria na mifumo ya ubora katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
"Mamlaka inatekeleza jukumu la usimamizi na udhibiti wa kemikali kupitia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Sheria Na. 3. ya Mwaka 2003. Lengo la Sheria hii ni kulinda afya na mazingira dhidi ya madhara ya kemikali," amesema.
Mkemia Mkuu ameongeza kuwa, utekelezaji wa sheria hiyo unafanyika kupitia usajili wa wadau, ukaguzi wa maghala na maeneo, ambapo kemikali zinatumika, ukaguzi wa maeneo ya mipaka ambayo mizigo yote ikiwemo kemikali zinapitia, na utoaji vibali vya kuingiza au kusafirisha kemikali ndani na nje ya nchi.
Amesema mamlaka imeendelea kufanya maboresho ya kuharakisha
mchakato wa usajili wa kampuni zinazojihusisha na biashara ya kemikali.
Kwa mujibu wa Mkemia Mkuu, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia, kumekuwa na ukuaji wa biashara ya kemikali, ambapo waliosajiliwa wameongezeka kutoka 2,125 mwaka 2021 hadi 3,835 kufikia Juni 2025, sawa na ongezeko la asilimia 81 la wadau waliosajiliwa.
"Mamlaka hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maghala yanayohifadhi kemikali na maeneo ya mipaka, katika kipindi cha miaka minne imekagua maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali sawa na asilimia 119 ya lengo la kukagua maghala 7,160," amesema.
Dkt. Mafumiko amesema Mamlaka imedhibiti uingizaji na usafirishaji wa kemikali hatarishi na zile zinazodhibitiwa chini ya mikataba ya kimataifa, ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na usalama wa nchi, kwa kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali hizo.
Amesema kumekuwa na ongezeko la vibali vya uingizaji wa kemikali kutoka vibali 40,270 kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 hadi 67,200 kufikia Mwaka wa Fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 40 ya vibali vilivyotolewa.
"Ongezeko la vibali limetokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita, wadau kuongeza uelewa wa sheria, kanuni na miongozo inayosimamia shughuli za kemikali kwa kujengea uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya tehama, inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali," amesema.
Amesema Mamlaka imeendelea kuchangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini, hasa za kimkakati zinazotumika kwenye uchimbaji na uchenjuaji wa madini ndani na nje ya nchi, zikiwemo Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mkemia Mkuu huyo ameongeza kuwa, Kemikali ya Ammonium Nitrate inayotumika katika ulipuaji wa miamba wakati wa uchimbaji madini, imeongezeka kutoka Tani 135,445 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi Tani 461,777.42 kufikia Juni 2025, sawa na ongezeko la asilimia 241.
Amesema Mamlaka imewezesha zaidi ya asilimia 80 ya shehena ya Ammonium Nitrate iliyoingizwa nchini, kupitia bandari ya Tanga, hivyo kuongeza thamani ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kuongeza kina cha bandari hiyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mafumiko, wakati kemikali ya Salfa inayotumika katika mchakato wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya shaba nchini Zambia na DRC, ambayo hupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka Tani 396,982 Mwaka Fedha 2021/2022 hadi Tani 1,867,104.72 kufikia Juni 2025, sawa na ongezeko la asilimia 370.32.
"Kemikali ya Sodium Cyanide inayotumika katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu nchini na nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo uingizwaji wake hupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kutoka Tani 41,461 Mwaka Fedha 2021/2022 na Tani 63,103.4 kufikia Juni 2025 sawa na ongezeko la asilimia 52.20.
Ametaja sababu za kuongezeka kwa uingizaji wa kemikali hizo kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga, kuwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya bandari na mahusiano mazuri kati ya Tanzania na nchi jirani yaliyowekwa na Serikali.
"Kupitia mpango wa elimu kwa umma unaotekelezwa na Mamlaka kwa wadau wa biashara ya kemikali, kumekuwa na ongezeko kubwa la wadau wanaotimiza matakwa ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali, kuboresha miundombinu wezeshi ya ofisi na maabara za uchunguzi na ujenzi wa Jengo la Mamlaka Makao Makuu - Dodoma," amesema.
Dkt. Mafumiko amesema kuwa, Mamlaka imefanikiwa kujenga, kukamilisha na kuanza kutumia jengo lake Makao Makuu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, eneo la Medeli jijini Dodoma, ambapo ujenzi wa jengo hilo umegharimu Sh. bilioni 8.14.Amesema jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia maabara tano, wakati hivi sasa maabara tatu zinafanya kazi, baada ya ununuzi na usimikaji wa mitambo ya uchunguzi wa kimaabara ya kisasa kukamilika.
Amezitaja maabara hizo kuwa ni Maabara ya Uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu, Maabara ya Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyama Pori na Maabara ya Sayansi Jinai Kemia na Toksikolojia.
"Mamlaka imeendelea kutengeneza, kujenga na kusimika mifumo mbalimbali ya tehama kupitia watalaam wake wa ndani, mifumo hii imeimarisha na kuongeza matumizi ya tehama ndani ya Mamlaka kama Mfumo wa Usajili na Utoaji Vibali kwa Wadau wa Kemikali, ambao umeongeza ufanisi na kupunguza muda wa kutoa vibali kutoka siku saba hadi muda wa ndani ya saa moja.
"Pia kuna Mfumo wa Kutoa Ushahidi kwa Ki-electroniki, unaolenga kupunguza gharama kwa Serikali kwa wataalam kusafiri kwenda kutoa ushahidi mahakamani kwenye mnyororo wa haki jinai,” alisema.
Alitaja mfumo mwingine kuwa ni Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Watoa Ushahidi Mahakamani, unaosaidia ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama kupata taarifa za mwenendo wa watoa ushahidi wataalam kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Amesema ujenzi na usimikaji wa mifumo hiyo, umetumia wataalam wa ndani wa Mamlaka kwa kushirikiana na wataalam wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), wakati katika kuboresha ufanisi, tija na utendaji kati ya taasisi za Serikali, Mamlaka imefanikiwa kujenga mifumo ya tehama yenye uwezo wa kubadilishana taarifa kwa mujibu wa maekelezo ya Serikali."Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa za Maabara, unaiwezesha Mamlaka kubadilishana taarifa na taasisi nyingine za haki jinai, kupitia mfumo huo Mamlaka imeungana na Mfumo wa Jeshi la Polisi Tanzania na Mfumo wa Serikali wa Kubadilishana Taarifa (GovESB), ili kuboresha ufanisi na utendaji kazi wa mfumo wa haki jinai nchini," amesema Mkemia Mkuu, Dkt. Mafumiko.
Ameongeza kuwa, Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa za Wateja wa Kemikali, umeunganishwa kwenye Mfumo wa Serikali wa Kubadilishana Taarifa na Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wa Ugomboaji Mizigo kwa pamoja na Mfumo wa Malipo wa Serikali, ili kuwezesha malipo na utoaji mizigo bandarini kwa wakati na kuongeza ufanisi na tija kwa Serikali.
Dkt. Mafumiko amesema katika kuhakikisha usalama wa ubadilishanaji taarifa, Mamlaka imeunganisha ofisi zake zote za Kanda na Mfumo wa Mawasiliano wa Ndani kwenye Mfumo Mkuu wa Mawasiliano wa Serikali, hatua hiyo iliyoiwezesha Mamlaka kupata huduma ya mifumo ya pamoja ya Serikali kama e-Office kwa usalama na kuhakikisha ubadilishanaji wa taarifa unafanyika katika miundombinu salama ya Serikali.
Amesema katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2021/2022 hadi Machi, 2025, Mamlaka imetoa mafunzo kwa wadau 1,201 wa mnyororo wa haki jinai kama Mahakama, Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).
Wadau wengine ni waendesha mashitaka, hospitali na ustawi wa jamii na lengo ni kuhakikisha sampuli zinachukuliwa, zinatunzwa na kusafirishwa kwa usahihi bila kuathiri ubora wake pamoja na matokeo ya uchunguzi wake.
"Mamlaka pia imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wadau wa kemikali wanaosafirisha, wanaohifadhi, wanaotumia na kuteketeza kemikali, ili kulinda afya na mazingira dhidi ya madhara ya kemikali. Tumetoa mafunzo hayo kwa wadau 12,689 kuanzia Mwaka 2021/2022 hadi Machi, 2025."
Ametaja wadau walionufaika na mafunzo hayo, kuwa ni madereva 6,358 waliopatiwa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali ndani na nje ya nchi, wasimamizi 5,036 wa shughuli za kemikali katika maeneo ya bandari kavu, maghala na wasimamizi wa maeneo ambayo kemikali zinatumika na kuhifadhiwa.
Ameongeza kuwa, wengine walionufaika na mafunzo hayo ni wadau 29 wenye changamoto ya usikivu waliopatiwa mafunzo ya usimamizi na utunzaji salama wa kemikali na viongozi wa Chama cha Madereva Wanaosafrisha Kemikali 65, walipatiwa Mafunzo ya Usafirishaji Salama wa Kemikali.
Mkemia Mkuu amesema kuwa, mamlaka imeendelea kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali, ikiwa ni sehemu yake kuchagiza maendeleo ya nchi, ambapo katika kipindi cha miaka minne, imechangia Sh. bilioni 3.9 kupitia maduhuli yaliyokusanywa na mamlaka hiyo.Dkt. Mafumiko amesema katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya Awamu ya Sita, Mamlaka katika miaka minne mfululizo mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025, imepata hati safi za ukaguzi wa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
"Kutokana na utendaji mzuri, Mamlaka inategemea kuendelea kupata hati safi kwa kuendelea kuboresha na kuongeza ufanisi katika utendaji wake wa kazi," amesema.
Mkemia Mkuu amesema kuwa, matarajio ya Mamlaka ni kuendelea kuimarisha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa sampuli na utoaji matokeo ya uchunguzi kwa wakati, ikiwemo ununuzi wa mitambo ya uchunguzi, ili kukabiliana na changamoto ya kukua na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Pia, kuendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani kwa kuimarisha matumizi ya tehama, kuendelea kukamilisha miundombinu wezeshi kwa kujenga majengo yake ya ofisi na maabara katika kanda kwa lengo la kusogeza huduma zitolewazo na mamlaka karibu na wananchi, na kuendelea kuimarisha matumizi ya tehama na kuifanya kuwa Mamlaka Janja.
"Usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na
majumbani, kuboresha matumizi ya tehama katika usimamizi na menejimenti ya
taarifa za maabara, ili kutoa matokeo kwa haraka na kwa usahihi zaidi.
“Pia kuboresha mifumo ya pamoja ya Serikali katika kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha, usimamizi wa rasilimali watu na mifumo ya uratibu wa majukumu, Mamlaka itapata fursa ya kupunguza makosa ya kibinadamu na kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu na itasaidia kufikia malengo kwa haraka zaidi na kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Matarajio mengine amesema ni kuwezesha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa kwa kuwezesha mifumo kusomana na kubadilishana taarifa na taasisi nyingine ikiwemo haki jinai, kuimarisha usalama wa data na taarifa ili kulinda taarifa za Serikali na wadau, kutoa elimu kwa umma na wadau wa shughuli za Mamlaka ili kuviwezesha vyombo vya utoaji wa haki, huduma ya afya na mazingira.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni mojawapo ya
taasisi za Serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali, Sheria Na. 8 ya mwaka 2016. Kabla ya hapo, taasisi hii
ilikuwa ni mojawapo ya Wakala na Serikali chini ya Sheria ya Wakala za Serikali
Na. 30 ya Mwaka 1997 ikitokea kuwa mojawapo ya Idara ndani ya Wizara ya Afya.
No comments