Header Ads

ad

Breaking News

Dira ya Taifa 2050 ina ulinzi ya marais wanne kuitekeleza

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imekamilika ambapo inatarajiwa kuzinduliwa na  Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 17, mwaka huu. 

Prof. Mkumbo amesema mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ulizinduliwa Aprili 3, 2023 na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na kuanza mchakato wa kuunda vyombo vya kitaasisi vya kusimamia uandishi wa Dira. 

Profesa Mkumbo amewaeleza wahariri na waandishi wa habari kuwa, mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, baada ya kupitia hatua 12 zilizotakiwa, imekuwa ni Dira ya Pili ya Maendeleo ya Taifa, ambayo haina uelekeo wa kiitikadi katika chama.Amesema uzinduzi wake utafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete mjini Dodoma, ambapo wadau mbalimbali wa maendeleo watashuhudia tukio hilo la kihistoria la kuwa na Dira 2050, wakati Rais, Dkt. Samia atakapokuwa Rais wa pili nchini kuandika dira ya maendeleo. 

Profesa Mkumbo amesema Rais Dkt. Samia, atazindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo yaani Dira 2050, Alhamisi ya  Julai 17, 2025.

Amesema ni mara ya pili nchi  kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo, wakati huko nyuma kulikuwa na Dira ya Azimio la Arusha ambayo ilikuwa ni dira kamili ya kitaifa, ikiwa ni Programu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya miaka 15 kuanzia   2007 hadi 2002. 

Ametaja sifa yake ya kuwa haina mwelekeo wa kiitikadi ya chama chochote cha siasa, kwani zilizopita zilikuwa na mwekekeo wa itikadi ya chama, ambapo Azimio la Arusha lilikuwa la CCM, wakati wa chama kimoja na nyingine ilikuwa programu ya chama hicho, lakini dira ya kwanza isiyo na mwekekeo wa chama ni Dira 2000 - 2025. 

“Rais Samia anakuwa wa pili kuandika dira, akitanguliwa na Benjamin Mkapa, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu. tunampongeza Dkt. Samia kwa kupata heshima ya kuandika dira itakayoongoza nchi kwa miaka 25," amesema. 

Profesa Mkumbo amesema Desemba 9, 2024 alikutana na wahariri wa vyombo vya habari kutoa taarifa ya hatua ambayo imefikia katika maandalizi ya Dira ya Taifa, ambapo aliwapa taarifa kuwa, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi atazindua Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo  tayari aliizindua na sasa Julai 8, 2025 kupitia wahariri, umma uwe na taarifa wamefikia wapi maandalizi ya dira na hatua gani inafuata. 

Prof. Mkumbo amesema maandalizi ya ya dira yamepitia hatua muhimu 13, ambapo hadi sasa wamepita hatua 12 na kubaki moja.

Alitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni Kuandaa na Kuidhinishwa   miongozo ya 2050 na Aprili 3,2023, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, kwa niaba ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi mchakato wa kuanza kuandika dira. 

Amesema mchakato huo ulianza Aprili 3, 2023 na Aprili 3, 2025 umetimiza miaka miwili na miezi minne, wakati hatua ya tatu ilikuwa kuunda vyombo vya kitaasisi vya kusimamia uandishi wa dira. 

Profesa Mkumbo amesema mchakato wa uandishi wa Dira umepita katika hatua tatu;  kwanza kulikuwa na Sekretarieti ya Kuandika Dira, Timu Kuu ya Kitalaam ya kuandika dira na chombo cha tatu ilikuwa Kamati ya Uongozi wa Dira,  ambayo ilikuwa chini ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mwenyekiti Mwenza Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla. 

Amesema hatua nyingine ilikuwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya ya Taifa ya Maendeleo ya 2000-2025, ambapo tangu mwaka 2000, Serikali na wadau wengine wa maendeleo walikuwa wakiongozwa na Dira ya Taifa ya 2000-2025, lakini kabla ya kufanya uandishi, ilikuwa lazima ifanyike tathmini ya utekelezaji wa dira kuona mafanikio na changamoto zake. 

“Ripoti ya taarifa hii ya tathimini ilizinduliwa rasmi Desemba 9, 2023 kwenye Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira na Mgeni Rasmi alikuwa Rais Samia, alizindua rasmi pia nyenzo ya kukusanya maoni ya wananchi na wadau kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema. 

Amesema mkutano wa kwanza ulifanyika Desemba 9, ukiwa na majukumu mawili; Kufanyika Taarifa ya Tathimini ya Dira ya Maendeleo, Kuzindua Timu Kuu ya Kitalaam na Uzinduzi wa Nyenzo ya Kukusanya Maoni ya Wadau. 

Amesema hatua ya tatu ilikuwa kukusanya maoni ya wananchi na wadau wa maendeleo kuhusu matarajio yao, maudhui gani yaingizwe katika Dira ya 2050, ambapo zoezi hilo lilikuwa shirikishi nchi nzima huku likigusa kila mwananchi na kufanikiwa kuwafikia watu milioni 1.2. 

“Sampuli katika tafiti ni watu 5,000 na wakizidi sana 10,000, lakini nyingi ni 2,000 au 3,000, mchakato wa Dira ya Maendeleo umewafikia watu zaidi ya milioni 1.2 na tulitumia njia saba, ikiwemo kufanya tafiti kuanzia ngazi ya tawi," amesema. 

Profesa Mkumbo amesema hatua nyingine ya mchakato huo wa kuandaa dira, imepitia mchakato wa maamuzi ndani ya Serikali, ambapo Juni 22, mwaka huu waliifikisha kwenye Baraza la Mawaziri na kuidhinisha rasmi dira ya maendeleo. 

“Juni 22, 2025 ni siku muhimu, ni siku Baraza la Mawaziri lilipitisha rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo na kuipeleka Bungeni  ambako iliridhiwa.

“Tofauti na dira inayoisha muda wake, iliidhinishwa na Baraza la Mawaziri na kumalizikia hapo, lakini mwaka huu, Rais Dkt. Samia alielekeza lazima ipelekwe bungeni, lengo lake ni kuweka ulinzi," amefafanua. 

Meneja mawasiliano na uhusiano Tume ya Mipango, Titus Kaguo

Profesa Kitila amesema dira hiyo itatekelezwa na marais wasiopungua watatu hadi wanne, hivyo Dkt. Samia anakuwa wa kwanza kuisimamia hadi mwaka 2030, wakati atayefuata atakaa miaka 10, ambapo atatoka mwaka 2040.

Mwingine akikaa miaka 10, atatoka madarakani mwaka 2050, hivyo marais wasiopungua watatu wataisimamia Dira ya Taifa 2050. 

Waziri huyo amesema Rais alifanya uamuzi sahihi wa kuwataka waipeleke bungeni, lengo likiwa kuweka ulinzi, kwani ikipelekwa huko ikihitajika kubadilisha chochote, lazima irudishwe Bungeni. 

Amesema hatua iliyobakia ni kuutaarifu umma kupitia mchakato wa maandalizi ya dira ya maendeleo kuwa, umekamilika na Dira ya Taifa ya Maendeleo itakayojulikana kama Dira 2050, ipo ikiwa kwa Kiswahili na Kiingereza.









No comments