Header Ads

ad

Breaking News

Wakazi Kwaruhombo wakosa maji kwa muda mrefu

Na Omary Mngindo, Mbwewe

WAKAZI wa Kijiji cha Kwaruhombo Kata ya Mbwewe Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanatumia maji ya visima kwa zaidi ya miaka kumi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Kwaruhombo, Kijiji cha Kwaruhombo, Aweso Kigonile  alisema tangu wawekewe vibanda kwa ajili ya kuchotea maji, hawajawahi kupata hudfuma lakini hakuna huduma hiyo.

"Maji yalipatikana ulipozinduliwa mara ya kwanza miaka hiyo, mpaka sasa maji hayatoki hivyo, wananchi tunateseka. Huku tunatuma maji ya visima ambayo si safi na salama," alisema Kigonile.

Mohamed Salum alisema tangu walipojengewa vibanda sita kijijini hapo hadi sasa hakuna maji, huku akisikitishwa na uwepo wa mabomba mabovu waliyopelekewa wakati maeneo mengine maji yanatoka.

"Wanatuletea mabomba mabovu tunapowaambia wanasema wataleta mengine, lakini miaka inakatika, hapa kijijini kwetu wamejenga vibanda sita kwa ajili ya huduma hiyo, lakini tunatumia maji ya visima pamoja na mifugo," alisema Salum.

Mohamed Chambega alisema kuwa, pamoja na uwepo wa miundombinu ya huduma hiyo lakini maji hayatoki "Tangu iwekwe miundombinu hiyo, maji yalitoka siku ya kwanza ya mradi, toka hapo hayatoki mpaka leo," alisema Chambega.

"Wanatuletea mabomba mabovu ambayo hayana msaada kwetu, pamoja na hilo tunaendelea kutaabika kwa kukosekana huduma hiyo muhimu," aliongeza Chambega.

Meneja wa DAWASA Chalinze, Mhandisi Abraham Mwanyamaki alielezea kushtushwa kwa taarifa hiyo, huku akisema atawaunganisha na anayesimamia miradi hiyo kwa ufafanuzi zaidi juu ya changamoto hiyo.

"Hiyo taarifa ndiyo naisikia kwako, nitamwambia mhandisi anayesimamia miradi ili akupatie ufafanuzi zaidi, ndiyo naisikia kutoka kwako," alisema Mhandisi Mwanyamaki.

Akizungumzia adha hiyo, Mhandisi anayesimamia mradi alikiri kuwepo kwa adha hiyo, huku akieleza kuwa yeye ni mgeni Chalinze,  lakini wiki iliyopita alifika na kujionea kilio hicho na kwamba, atawaambia vijana wake wafuatilie.

"Kuanzia Jumatatu tutaanza kufuatilia, kuna eneo linaitwa Kifuleta Mtoni kuna bomba limeoza tumeanza kulifuatilia ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi," alisema.

Aliongeza kuwa, "Mradi huo ulikuwa chini ya CHALIWASA, tatizo tunalitambua hivyo kuanzia Jumatatu tutaanza kupambana nalo, wakati wowote adha hiyo itapatiwa ufumbuzi," alimalizia Mhandisi huyo.


Tatizo la maji Chalinze limekuwa sugu, ambapo pamoja na juhudi za serikali kuupeleka mradi mkubwa unaotoka Mtambo wa Ruvu Juu uliogharamiwa kwa fedha nyingi, bado wananchi wanakabiliwa na adha kubwa ya huduma hiyo muhimu.


No comments