Bunge lampa tuzo Rais Samia, CCM yampongeza kongole
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezi na chama hicho kwa heshima kubwa aliyopewa na Bunge ya kutunukiwa Tuzo Maalum ya Heshima.
Tuzo hiyo, iliyokabidhiwa rasmi na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson juzi, ni kielelezo kingine cha kuthibitisha mchango mkubwa, wa kipekee na wenye matokeo chanya wa kazi nzuri zilizofanywa na Rais Dkt. Samia katika kulijenga Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Halmashauri ya CCM, Itikadi na Mafunzo, CPA. Amos Makalla amesema tuzo hiyo ni ushahidi wa wazi wa kuthaminiwa kwa uongozi wake madhubuti, unaojengwa juu ya misingi ya amani, maridhiano ya kisiasa, mshikamano wa kitaifa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa Watanzania wote.
“Ni matokeo ya utekelezaji wenye mafanikio makubwa wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Tunajivunia kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea kudhihirisha uimara, umakini na weledi wa chama katika kutoa uongozi thabiti kwa nchi yetu. Ni fahari kwa CCM kuwa na kiongozi mwenye maono, uthubutu na dira ya maendeleo jumuishi kwa wote,”amesema.
Amesema kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi na wananchi wapenda maendeleo na amani nchini, amemhakikishia Rais Dkt.Samia ushirikiano wa dhati, mshikamano usiotetereka na uungaji mkono muda wote anapotimiza wajibu wake kwa watanzania wote.“Tuzo hii inaungana na heshima nyingine nyingi alizopokea Rais ndani na nje ya nchi, kama ishara ya kutambua mchango wake wa kipekee katika kuimarisha utawala bora, kuhimiza maendeleo shirikishi na kuendeleza taswira chanya ya Tanzania kimataifa,”amesema.
Ameongeza kuwa, CCM ina imani kubwa na uongozi wa Rais Dkt. Samia, katika kuliongoza Taifa letu kwa amani, ustawi na mafanikio ya kweli.
No comments