Header Ads

ad

Breaking News

CHAURU hatarini kukosa mavuno, tuta lazilewa na mafuriko

Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU), Otiniel Mbura

Na Omary Mngindo, Vigwaza

USHIRIKA wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU), kinachofanya shughuli za kilimo katika Kitongoji cha Mlelani Kijiji cha Visezi Kata ya Vigwaza, Chalinze Bagamoyo Pwani kipo hatarini kukosa mavuno.

Hali hiyo inachangiwa na kubomoka kwa tuta linalosaidia kuingiza maji kwenye skim hiyo, yanayokwenda kusukumwa na pampu ya ushirika huo na kuingia katika mashamba.

Makamu Mwenyekiti wa ushirika huo, Otiniel Mbura, alisema kwamba tuta hilo ni kiungo muhimu katika Ushirika wao, huku akiiomba serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuangalia ni namna gani ya kuwashika mkono.

"Lile tuta ndiyo roho yetu sisi kwani, linachangia kuingiza maji ndani ya Ushirika, kisha pampu ikiwashwa inasambaza maji kwenye mashamba ya wanachama," alisema Mbura.

Alisema kuwa ili kulirejeshwa katika hali ya kawaida, yanahitajika mamilioni ya shilingi kuweza kuendelea kuwapatia huduma wana CHAURU hao.
Mjumbe wa Bodi ya Ushirika wa Umwagiliaji Ruvu (CHAURU), Sheha Zuberi 

Mjumbe wa Bodi ya Ushirika huo, Sheha Zuberi alisema kuwa kuna baadhi ya mashamba tayari mpunga umeanza kuchanua, huku mengine yakianza kupandikizwa.

"Tunaiomba serikali ituangalie kwa jicho la haraka ili kukabiliana na athari iliyopo, kwani kinyume chake kwa kasi ya maji yanayoingia bila mpangilio tuna hofuya kuathiriwa hata kwenye makazi," alisema mjumbe huyo.

Mwanachama Abdallah Mbangwi alisema kuwa kutokana kadhia hiyo ameiomba Halmashauri ya Chalinze kuangalia kupitia mfuko wa dharula wawakimbilie ili kunusuru ushirika wao.

"Nadhani upande wa Halmashauri kuna mfuko wa maafa, ingekuwa jambo jema wakatukimbilia katika kupambana na changamoto iliyotukuta, kwani kinyume chake Hali itakuwa mbaya zaidi," alimalizia Mbangwi.

No comments