CCM LONDON DIASPORA WAZURU KABURI LA HAYATI ABEID AMANI KARUME, WAMSOMEA DUA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAJUMBE Chama Cha Mapinduzi CCM Tawi la London Diaspora la nchini Uingereza wamezuru Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume lililopo kando ya Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) eneo la Kisiwandui Zanzibar.
Wanadiaspora hao wameshiriki dua ya kumuombea Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume na kuombea amani katika kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Wajumbe hao, wakiwa chini ya uongozi wa viongozi wakuu wa CCM kutoka Uingereza na Wanadiaspora, wameongozwa na Mwenyekiti wa msafara huo Haruna Rajabu Mbeyu waishio London, na wamepata wasaha kuhusu historia ya Hayati Karume, Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na chimbo la vyama vya siasa Zanzibar na baadae CCM.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa msafara huo, Bw Haruna Mbeyu ambaye pia ameongoza Dua hiyo maalum kumuombea Hayati Sheikh Abeid Amaan Karume amesema kuwa, wamefika visiwani Zanzibar kuendelea kujifunza mambo mbali mbali ya Chama na Serikali pamoja kuenzi waasisi wa Taifa wa pande zote mbili Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wana Diaspora hao wapo Visiwani Zanzibar kuanzia Juni 3, 2025
Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na mahusiano kati ya wanadiaspora wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) sambamba na kujadili fursa mbalimbali za maendeleo na mchango wa Diaspora katika maendeleo kupitia Chama Cha Mapinduzi.
No comments