Header Ads

ad

Breaking News

Sekta ya madini yazidi kupanda Pato laTaifa

Waziri wa Madini Anthony Mavunde akiwasilisha taarifa za mafanikio ya sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Mei 24,2025

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarika na kukua katika Pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021, asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024. 

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mei 24,2025, Waziri Mavunde, amesema sekta ya madini imefanikiwa kuvuka lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa mwaka mmoja kabla ya muda ulioainishwa katika Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026 na kufikia mchango wa asilimia 10.1 mwaka 2024. 

Amesema kasi ya ukuaji wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 mwaka 2021, asilimia 10.8 mwaka 2022 na kufikia asilimia 11.3 mwaka 2023. 

Waziri avunde amesema kuwa, serikali imeendelea kuboresha sheria, kanuni na miundombinu mbalimbali ikiwemo umeme migodini, ambapo imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza ufanisi wa kazi katika shughuli za madini. 

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Yahya Samamba akizungumza wakati wa mkutano wa wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

Amesema kutokana na ushirikiano uliokuwepo, maduhuli ya serikali yamepanda kutoka shilingi bilioni 623.24 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 753.18 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 20.8 ya makusanyo kwa miaka mitatu, na kwamba Wizara hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, ilipewa lengo la kukusanya shilingi trilioni moja.

 "Hadi kufikia Mei 14,2025, Wizara ya Madini tumefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 902.78 sawa na asilimia 90.28 ya lengo la mwaka 2024/2025," amesema Waziri Mavunde.

Ameongeza kuwa, mchango wa sekta ya madini katika fedha za kigeni kwa mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi umeendelea kuimarika kutoka Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na asilimia 45.9 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 3.55 sawa na asilimia 46.1 mwaka 2023. 

Wazir Mavunde amesema kwamba, mauzo ya bidhaa zisizo asilia, mchango wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 53.8 mwaka 2021 hadi asilimia 56.2 mwaka 2023. 

Mhariri wa gazeti la Raia Mwema na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Joseph Kulangwa akiuliza swali

Waziri Mavunde amesema bajeti ya Wizara ya Madini imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, kutoka shilingi bilioni 89 kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 hadi shilingi bilioni 231 kwa mwaka 2024/2025, ambapo Mwaka wa Fedha 2025/2026, wameidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 224. 

Amesema kiasi kikubwa cha bajeti hiiyo kimeelekezwa kwenye Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), wa lengo la kufanya tafiti za kina za jiolojia na ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchambuzi wa madini katika eneo la Kizota mkoani Dodoma. 

"Madhumuni yetu ni kuifanya GST kuwa kitovu cha huduma za maabara ya madini kwa Afrika nzima, pia, maabara nyingine zinajengwa katika mikoa ya Geita na Chunya mkoani Mbeya ili kuboresha huduma za uchambuzi wa madini nchini," amesema Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde amesema mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa (GDP), umeongezeka kwa kiwango kikubwa, ambapo sera ya madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo kwa Miaka Mitano unalenga sekta hiyo kuchangia angalau asilimia 10 ya GDP ifikapo mwaka 2025. 

Amesema hadi kufikia Desemba 2024, mwaka mmoja kabla ya muda uliopangwa, sekta ya madini imefikia mchango wa asilimia 10.1, ambayo ni hatua nzuri kwa wizara na taasisi zake.

Waziri Mavunde amesema hivi sasa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza rasmi kununua dhahabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani, baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2024. 

"Baada ya marekebisho ya sheria ya madini mwaka 2024, hivi sasam Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imeanza kununua dhahabu kutoka kwa wazalishaji, kwetu ni Faraja kubwa sana," amesema.

"Sheria hivi sasa inawataka wamiliki wote wa leseni za uchimbaji wa dhahabu kutenga angalau asilimia 20 ya uzalishaji wao kwa ajili ya kuuza BOT." 

Waziri Mavunde amesema kuanzia Oktoba 2024 hadi sasa, BoT imenunua tani 3.7 za dhahabu. Kwa hatua hii, Tanzania inajiweka kwenye nafasi nzuri kuwa miongoni mwa nchi zenye akiba kubwa ya dhahabu barani Afrika, ikitanguliwa na Algeria yenye akiba tani 174, na Msumbiji nafasi ya 10 ikiwa na tani 3.6.

Ameongeza kuwa, kutokana na sera na usimamizi mzui wa sekta ya madini, wachimbaji wadogo wanachangia asilimia 40 ya mapato yote yatokanayo na sekta ya madini. 

"Serikali imefuta leseni na maombi 2,648 ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata maeneo halali ya uchimbaji, na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limejipambanua kuwa mlezi wao na tayari limewanunulia mashine 15 za kuchoronga miamba." 

Amesema kuwa, Wizara imeunda timu ya wataalam sita kutoka sekta binafsi na serikali kwa ajili ya kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuwainua wachimbaji wadogo, ikiwa pamoja na kufanya mazungumzo na benki mbalimbali ili kuhamasisha kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo, ambapo sasa wanakopesheka. 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akiuliza swali


Ameongeza kuwa, eneo la mgodi wa Buzwagi unaofungwa baada ya kusitisha shughuli za uchimbaji limegeuzwa kuwa eneo maalum la uwekezaji wa viwanda, moja ya viwanda vitakavyojengwa ni kiwanda cha kusafisha makinikia cha Tembo Nickel Refining Limited, kitakachokuwa kikiongeza thamani ya madini ya nickel na ajira nchini.

"Serikali imerejesha rasmi minada ya ndani ya madini ya vito kwa lengo la kuongeza thamani ya madini haya, hasa Tanzanite ambayo ni adimu duniani, tayari tumefanya minada Mirerani Desemba 2024 na Arusha Februari 2025," amesema.

Waziri Mavunde amesema katika kuwapigania wachimbaji wadogo,  wamefanya marekebisho ya Sheria mwaka 2024, ambayo inaeleza kuwa, leseni za uchimbaji mdogo wa madini ni kwa ajili ya watanzania pekee. 

Kuhusu STAMICO, Waziri Mavunde amesema kuwa, shirika la hilo limepiga hatua kubwa kutoka kuingiza mapato ya shilingi bilioni 1 hadi shilingi bilioni 84, ndani ya kipindi cha miaka minne, ambapo limefanikiwa kujilipa mishahara lenyewe, linatoa gawio serikalini na limepanga kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati kuanzia mwaka wa fedha ujao ili taifa linufaike zaidi. 

Waziri Mvunde amesea kuwa, ajira kwa wazawa sekta ya madini zimeongezeka, za moja kwa moja ni zaidi ya 19,356, asilimia 97 ya ajira ni wazawa, wengine wakishikilia nafasi nyingi za juu kwenye migodi. 

Aidha, amesema serikali iko mbioni kukamilisha mkakati maalum wa namna ya kuyavuna na kuyaendeleza madini mkakati kama vile graphite, nickel, rare earths kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mhariri na mmiliki wa Fullshangwe Blog, John Bukuku akiuliza swali katika mkutano huo

"Serikali ipo kwenye mazungumzo na Benki Kuu ya Tanzania kuhusu kuanzisha sarafu za dhahabu (Gold Coins), kwa ajili ya uwekezaji na akiba ya thamani. Lengo ni kuwawezesha watanzania kuhifadhi dhahabu benki na kuitumia kwa malipo kama vile mafuta ya petroli na dizeli."

Amesema Wizara ya Madini imesaini mikataba ya ushirikiano na nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza, Sweden, Finland na nyingine nyingi kwa ajili ya kukuza ujuzi, teknolojia na kupata mitaji kwa ajili ya maendeleo ya sekta kwa manufaa ya taifa.

"Mwaka 2017, serikali ilisitisha minada ya ndani ya madini ya vito na maonesho ya madini kwa lengo la kutafuta namna bora ya uendeshaji, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa  Tanzania (TMX) ilifanya mnada wa kwanza wa madini ya vito ndani ya nchi Desemba 14, 2024," amesema.

Amesema mnada wa pili ulifanyika Aprili 8, 2025 katika Mkoa wa kimadini wa Mirerani tangu kusitishwa mwaka 2017, katika minada hiyo, jumla ya wanunuzi 60 walipatikana kama washindi wa mnada na kufanikiwa kununua madini yenye thamani ya shilingi 2,509,245,216.00.

Ameongeza kuwa, minada hiyo iliiwezesha serikali kukusanya jumla ya shilingi 163,084,534.84 ikijumuisha mrabaha wa shilingi 149,218,787.80, ada ya ukaguzi ya shilingi 11,390,747.16, ada ya usimamizi wa mnada ya shilingi 2,509,245.22 na ada ya ushiriki wa mnada shilingi 6,850,852.50.

"Wizara kupitia Tume ya Madini tunategemea kufanya minada na maonesho ya kitaifa katika mikoa ya kimadini ya Arusha, Mirerani, Mahenge, Ruvuma na Tanga, wakati maonesho ya kimataifa yatafanyika Zanzibar, Dar es Salaam na Arusha," amesema.

Mhariri wa Raia Mwema, Suleiman Msuya akiuliza swali katika mkutano huo


No comments