Benny Mwaipaja,
WFM
SERIKALI imeipatia
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), sh. bilioni 209.5 kwa ajili
ya kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo hapa nchini, leo, Jijini Dar es salaam.
Akiongea kwa niaba
ya Serikali wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makabidhiano ya fedha
hizo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Khatibu Kazungu,
alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ni sehemu ya sh. bilioni 800, ambazo
Serikali inatarajia kuipatia Benki hiyo ili iweze kukuza mtaji wake.
“Ninaishukuru
Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa kuipatia Serikali mkopo wa Dola za
Marekani milioni 93.5 milioni ambazo ni sawa na kiasi hicho cha fedha cha sh. bilioni 209.5
kwa ajili ya kuiongezea mtaji TADB ili iweze kuwafikia wakulima wengi
zaidi kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu,” amesema Dk. Kazungu.
Amesema kuwa fedha
hizo zitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ujenzi
wa miundombinu ya sekta ya kilimo na mifugo ili kuongeza uzalishaji na tija
katika kilimo ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika ukuaji wa pato la
Taifa kuliko ilivyo sasa.
“Mwaka jana kilimo
ambacho kinategemewa na idadi kubwa ya Watanzania kilichangia wastani wa
asilimia 29.1 ya Pato la Taifa lakini tunataka kupitia Benki hiyo Sekta ya
kilimo iiwezeshe nchi kukua kiuchumi kwa zaidi ya asilimia 7 hadi 10 katika
kipindi kifupi kijacho,” ameongeza Dk. Kazungu.
Akiongea baada ya
kutia saini makubaliano ya kupokea fedha hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Francis Assenga, ameishukuru
Serikali kwa kuiongezea Benki yake mtaji utakaotumika kuendeleza Sekta ya
Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ufugaji nyuki.
Amesema kuwa kiasi
hicho cha fedha kitaiwezesha benki hiyo ambayo imekwisha wafikia wakulima zaidi
ya 3,700 hapa nchini, kuanza kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wakulima wadogo na
wa kati ili kuinua Sekta hiyo kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao
yatokanayo na kilimo na mifugo.
Ameihakikishia
Serikali kwamba Benki yake itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa matunda
ya fedha hizo yanaonekana na kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kuwakwamua wananchi wake katika
lindi la umasikini.
“Riba za Mikopo ya
Benki yetu ziko chini ikilinganishwa na Benki nyingine ambapo sisi tunatoza
asilimia 8 hadi 12 kwa wakulima wadogo na asilimia 15 kwa wakulima wa kati
wenye viwanda wakati viwango vya riba katika soko ni asilimia 18 na wakati
mwingine vinafika hadi asilimia 40.” amesema Assenga wakati akijibu maswali
ya wanahabari.
No comments:
Post a Comment