Atletico yachafua hali ya hewa Jangwani
Mchezaji wa timu ya Yanga Juma Abdul akijaribu kunyang'anya mpira
kutoka kwa beki wa timu ya Atletico Henry Mbazumutima kwenye mchezo wa
pili wa fungua dimba katika michuano ya kombe la Kagame inayoandaliwa na
shirikisho la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki CECAFA
inayofanyika jijini Dar es salaam Tanzania, Mpira umekiwasha na timu ya
Yanga imeambulia kipigo cha magoli 2-0 yaliyofungwa na mchezji Didier
Kavumbagu wa Atletico
Wachezaji wa timu za Yanga ya Tanzania na Atletico ya Burundi
wakichuana vikali katika mchezo wao uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa
jioni ya leo.
MABINGWA wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, Yanga, wameanza vibaya kampeni ya kutetea
ubingwa wao huo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Atletico ya Burundi katika mchezo uliofanyika jana kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimekuja wakati klabu hiyo leo ikifanya
uchaguzi wa kuziba nafasi zilizo wazi baada ya baadhi ya viongozi wake, akiwamo
Mwenyekiti Lloyd Nchunga kujiuzulu.
Bila shaka, kipigo hicho kitakuwa kimetia doa kampeni za
baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa leo ambao walikuwa wakijinadi kwa wanachama
wao kutokana na usajili walioufanya, waliouita ‘wa mauaji’.
Tofauti na matarajio ya wapenzi wa Yanga, timu yao jana ilicheza katika
kiwango cha chini mno, wakionekana kuwa wachovu hivyo kushindwa kuhimili
mikimikiki ya Atletico.
Pamoja na kuanza vyema mchezo huo, kadri muda ulivyokwenda,
wachezaji wa Yanga walizidi kuchoka na baadhi yao kujikuta wakikaba kwa macho.
Kwa kiasi kikubwa, mabadiliko yaliyofanywa kwa upande wa
beki wa kulia, Juma Abdul aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Ladislaus
Mbogo, yalionekana kuigharimu zaidi Yanga kwani wapinzani wao walitumia nafasi
hiyo kuelekeza mashambulizi kupitia upande huo wa kulia na kupata mabao yote
mawili.
Kwa ujumla, Yanga jana ilizidiwa mno na Atletico ambao
walijaza viungo mahiri na wenye nguvu kama
Claude Nahimana, Christian Mbilizi aliyeingia kipindi cha pili, Henry
Mbazumutima, Gael Duhayingavyi na wengineo.
Pia, washambuliaji wa Atletico kama Didier Kavumbagu
aliyefunga mabao yote mawili na Christopher Ndayishimye, walikuwa ni moto wa
kuotea mbali kwa mabeki wa Yanga, wakiwa na nguvu, stamina na vimo virefu
vilivyowawezesha kumiliki kirahisi mipira ya juu dhidi ya walinzi wa Yanga.
Kwa upande wa Yanga, viungo wake walionekana kuchoka, hasa
wale wakabaji ambao muda mwingi walikuwa wakiumaliza katika eneo lao badala ya
kupandisha timu hata pale walipokuwa nyuma kwa bao 1-0.
Rashid Gumbo hakucheza kama ilivyo kawaida yake, kama ilivyokuwa kwa Haruna Niyonzima ambaye mara nyingi
alikuwa akikaa muda mrefu na mpira kutokana na viungo wenzake kuchelewa
kufungua nafasi, lakini wakati mwingine akifanya hivyo kutokana na kujiamini
kupita kiasi na mwisho wa siku kujikuta akipokwa mpira au kuupoteza.
Shamte Ally aliyekuwa akicheza kama kiungo wa kulia, hakutoa
mchango wowote kama kiungo kwani muda mwingi alikuwa akicheza pembeni ambapo
alishindwa kufanya lolote kwani hakuna krosi yoyote ya maana aliyopiga, hilo likitokana na uzito
na kutokuwa makini, pale alipopata mpira.
Jerry Tegete aliyekuwa mshambuliaji wa kati wa Yanga,
hakufanya kile kilichotarajiwa na wapenzi wa Yanga kutokana na kukosa
ushirikiano kutoka kwa viungo wake, ambao mara nyingi walikuwa wakimpelekea
mipira miguuni badala ya kwenye njia.
Hamis Kiiza aliyekuwa mshambuliaji mwenza wa Tegete, naye
jana hakuweza kufurukuta mbele ya mabeki wa Atletico ambapo hakuwa akitoa
msaada wowote kwa timu pale aliopoteza mpira bahati mbaya hata kizembe.
Kwa ujumla, Yanga jana haikucheza kiushindani wakiwa kama mabingwa watetezi hali inayozua hofu iwapo timu hiyo
inaweza kutetea ubingwa wake.
Yanga: Yaw Berko, Juma Abdul/Ladislaus Mbogo, David Luhende,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Shamte Ally,
Rashid Gumbo/Nizar Khalfan, Jerry Tegete/Said Bahanuzi, Hamis Kiiza na Haruna
Niyonzima.
Atletico: Said Ndikumana, Francis Nongwe, Hassan Habizimana,
Emery Nimubona, Pierre Kwizera, Gael Duhayindavyi, Claude Nahimana/Christian
Mbilizi, Henry Mbazumutima/Ciza Hussein, Christopher Ndayishimye, Didier
Kavumbagu na Etienne Karekezi.
No comments