Header Ads

ad

Breaking News

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Wahasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Ashura Ally na Edna Sanga wakifuatilia mada ya kumbukumbu gani umeiacha katika eneo lako la kazi kutokana na matendo yako mazuri uliyoyafanya iliyokuwa inatolewa katika mkutano wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) unaofanyika jijini Arusha.

Na Mwandishi Maalumu, Arusha

JAMII imetakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya za mioyo yao mara kwa mara ili kubaini mapema matatizo ya moyo na kuanza matibabu kabla hayajawa makubwa.

Wito huo umetolewa leo jijini Arusha na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Engerasia Kifai wakati akieleza huduma zinazotolewa na taasisi hiyo katika mkutano wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA).

“Ni muhimu kupima moyo mara kwa mara ili kubaini matatizo mapema na kuepuka matatizo makubwa ya afya,” alisema Dkt. Kifai.

Dkt. Kifai alisema njia bora ya kuepuka magonjwa ya moyo ni kuzingatia mtindo wa maisha wenye afya, ikiwemo kuepuka matumizi ya bidhaa za tumbaku, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kula chakula bora na kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi.

“Katika ukuaji wa mwanamke, kuna mabadiliko mbalimbali ya ndani na nje ya mwili ikiwemo kuongezeka kwa uzito na changamoto kwa moyo. Ni muhimu kuzingatia vyakula unavyokula kwa kupunguza ulaji wa vyakula vya wanga, sukari na chumvi kupita kiasi”, aliongeza Dkt. Kifai.

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Engerasia Kifai wa taasisi hiyo wakifuatilia mada ya kumbukumbu gani umeiacha katika eneo lako la kazi kutokana na matendo yako mazuri uliyoyafanya iliyokuwa inatolewa katika mkutano wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) unaofanyika jijini Arusha.

Akifafanua kuhusu huduma zinazotolewa na JKCI, Dkt. Kifai alisema taasisi hiyo inatoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na mishipa ya damu kwa watoto na watu wazima, na imepanua huduma zake kwa kufungua kliniki katika maeneo ya Kawe, Oysterbay, Dar Group na Chato.

“Taasisi yetu inafanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo, tunatoa huduma za matibabu kwa wagonjwa waliopo majumbani, fiziotherapia, elimu ya lishe bora na pia tunafanya upimaji wa afya kwa vikundi mbalimbali,” alisema.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo waliopata huduma ya upimaji wa afya ya moyo waliipongeza JKCI kwa huduma inayozitoa na kuomba huduma hiyo iendelee kutolewa katika mikutano mingine.

“Nimepata huduma ya upimaji wa moyo na ushauri wa lishe. Huduma imekuwa nzuri na ya haraka ninashukuru sana, ninawaomba wenzangu watumie mkutano huu kujifunza mada mbalimbali zinazotolewa na kupima afya za miyo yao,” alisema Pendo Mwakibinga kutoka EWURA.

“Nimefanyiwa vipimo vya sukari, presha, urefu na uzito, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mfumo wa umeme wa moyo. Nashukuru kwani sasa najua hali ya moyo wangu," alisema Joyce Maduhu kutoka Benki ya Kilimo.

Huduma hizi za upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo zinazotolewa na JKCI katika mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa taasisi hiyo wa program yake ya kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo ijulikanayo kwa jina na Dkt.Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayowawezesha  wananchi kupata mapema  matibabu ya moyo.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Idrisa Ndende akimpima kiwango cha sukari kwenye damu Mhasibu aliyefika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa mkutano wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) unaofanyika jijini Arusha.
Wanachama wa Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wanachama wa chama hicho katika mkutano wao unaofanyika jijini Arusha. Picha na JKCI

No comments