Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
WANAMICHEZO nchini wamepewa wito wa kufanya vipimo vya moyo kabla ya kuanza mazoezi au michezo ili kubaini iwapo kuna matatizo katika mishipa ya moyo au valvu jambo linaloweza kuokoa maisha yao.
Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Bonanza lililohusisha michezo mbalimbali ikiwemo baiskeli, mpira wa miguu na netiboli, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amesema baadhi ya wanamichezo hupoteza maisha ghafla kutokana na matatizo ya moyo, hususan misuli na valvu.
“Tunawahimiza wanamichezo kupima moyo wao kabla ya michezo, ili kudhibiti hatari ya kupata mshtuko wa moyo. Wananchi pia wajitokeze kwenye hospitali mbalimbali kufahamu hali zao za kiafya,” amesema Dkt. Kisenge.
Ameongeza kuwa kujizoeza kufanya mazoezi kwa wastani wa dakika 30 kila siku kunasaidia kutoa jasho mwilini na kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza hususan ya moyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bonanza hilo, Dkt. Evarist Nyawawa, amesema michezo iliyofanyika ilishirikisha taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).“Michezo ni sehemu ya ulinzi wa afya na mwendelezo wa matibabu. Tulishindana na timu kutoka taasisi hizi na washindi wamepewa zawadi,” amesema Dkt. Nyawawa ambaye pia ni Daktari Bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Naye, kapteni wa timu ya netiboli ya JKCI, Mariamu Maarufu, amesema timu yao ilishinda dhidi ya MOI kwa kupata mipira 19 dhidi ya 13 na kuongeza kuwa ushindi huo umetokana na maandalizi makali na mazoezi ya mara kwa mara.
Kapteni wa timu ya mpira wa miguu ya MNH Hemed Mohamed, amesema michezo inaimarisha afya na kuleta ari kazini, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi ya kawaida kwa kila mfanyakazi.
“Michezo si burudani tu, bali ni sehemu ya kujenga afya ya moyo na kudumisha ari kazini,” ameongeza.
Bonanza hilo lilifanyika katika uwanja wa APC Hotel & Conference Centre, Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI, ambapo kabla ya bonanza hilo shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwa ni pamoja na upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanafunzi, uzinduzi wa kamati ya kupandikiza moyo na mdahalo wa wazi wa kutoa elimu ya utalii tiba kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment