Thursday, September 18, 2025

TUME YA MADINI YAWAPIGA MSASA MAWAKILI WA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TUME ya Madini imeanza mafunzo maalum ya siku nne kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwandishi wa Sheria na Ofisi ya Msajili wa Hazina yanayolenga kuongeza uelewa wa wajibu wa kisheria na usimamizi wa Sekta ya Madini nchini. Mafunzo hayo yanafanyika Jijini Dodoma kuanzia Septemba 15 hadi 18, 2025.

Akifungua rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel M. Maneno, Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Neema Ringo, amesema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu kwa mawakili wa serikali katika kutekeleza majukumu yao.

“Mafunzo haya yatawawezesha Mawakili wa Serikali kuelewa kwa kina wajibu wa kisheria wa Tume ya Madini chini ya Sheria ya Madini, Sura ya 123 [R.E. 2023], na hivyo kuongeza ufanisi katika kusimamia na kulinda rasilimali za madini nchini. Ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta hii,” amesema Neema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tume ya Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera, akibainisha kuwa sekta ya madini ni nguzo muhimu ya uchumi wa nchi.
“Sekta ya madini ni miongoni mwa sekta zinazochangia kwa kiwango kikubwa kwa ukuaji wa uchumi wa nchi, mapato ya Serikali na ajira kwa wananchi. Mafanikio yake yanategemea sana usimamizi madhubuti wa sheria na mshikamano wa kitaasisi,” ameongeza.

Awali, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema mafunzo hayo yataleta tija kubwa kwa Mawakili wa Serikali, kwani yatawajengea uelewa mpana wa shughuli za madini na kuwawezesha kutoa ushauri sahihi wa kisheria.

“Tunatarajia baada ya mafunzo haya, mawakili wetu watakuwa na uelewa wa kina wa masuala ya madini na hivyo kuongeza weledi wao katika utoaji wa ushauri wa kisheria kwenye mambo mbalimbali yanayohusu sekta hii,” amesema Mhandisi Lwamo.

Mafunzo haya yameandaliwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yakilenga kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za madini kwa maslahi ya Taifa.







No comments:

Post a Comment