Header Ads

ad

Breaking News

MAFUNZO YA ULIPAJI WA TOZO ZA MADINI YAWAWEZESHA VIJANA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA SEKTA YA MADINI

Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga

OFISI ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Taasisi za Kibenki, imeendesha mafunzo kwa vijana wa Halmashauri mbili za Wilaya ya Sumbawanga kuhusu ulipaji wa tozo za madini na faida za sekta hiyo kwa maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Upendo Mangali, ambaye amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za madini ili kunufaika kiuchumi na kijamii.

Aidha, amewasisitiza wachimbaji wadogo kuona umuhimu wa kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa na serikali, kuchangamkia fursa za kifedha kutoka taasisi za kibenki na kuwekeza katika madini ya ujenzi na viwandani yaliyopo katika maeneo yao.

“Sekta ya madini ni fursa kubwa kwa vijana. endapo mtashiriki kikamilifu, mtajiongezea kipato, mtaendeleza jamii zenu na pia kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi,” amesema Mangali.


Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wataalam wa Ofisi ya Madini Rukwa, mafunzo hayo yamelenga vijana wenye nia ya kuingia kwenye mnyororo wa thamani wa shughuli za madini hususan uchimbaji wa madini ya ujenzi, viwandani na uwekezaji mwingine unaohusiana na sekta hiyo.

Washiriki wamepatiwa elimu kuhusu fursa za uwekezaji kwa vijana katika sekta ya madini, ulipaji wa tozo za madini, faida za madini kwa maendeleo ya vijana na taifa, elimu ya usalama na afya pamoja na utunzaji wa mazingira, sambamba na madhara ya kutokulipa tozo kwa wakati.

Mafunzo haya ni mwendelezo wa mpango wa utoaji elimu kwa wadau wa madini mkoani Rukwa, ulioanza Agosti 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba 2025 katika wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga.

No comments