JKCI yapokea msaada wa vifaa vya fiziotherapia vyenye thamani ya Shilingi milioni 24
Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imepokea msaada wa vifaa tiba vya kutolea huduma ya fiziotherapia kwa wanamichezo vyenye thamani ya Shilingi milioni 24 kutoka kampuni za Physiocare Tanzania na Enovis ya Afrika Kusini.
Pamoja na kupokea msaada huo jana jijini Dar es Salaam, taasisi hizo pia zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wanamichezo kupitia program ya Sports Cardiology.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Naizihijwa Majani, alisema kusainiwa kwa makubaliano hayo kutawasaidia wanamichezo kupata huduma bora za upimaji na matibabu ya moyo.
“Ninashukuru sana kwa msaada mliotupatia, kuwepo kwa vifaa hivi vya kisasa vya fiziotherapia vinavyotumia umeme kutawasaidia wanamichezo watakaopata matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa upasuaji kuendelea na matibabu ya fiziotherapia.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Physiocare Tanzania Remla Shirima wakionesha mkataba wa makubaliano ya programu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo Sport Cardiology waliyoisaini leo jijini Dar es Salaam.
“JKCI kupitia washirika wetu kama vile Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunahakikisha afya za wanamichezo zinakuwa salama kwa kuwafanyia uchunguzi kabla ya kuingia katika mashindano mbalimbali na hivyo kuweza kugundua matatizo ya moyo kwa wanamichezo mapema kabla hawajapata madhara,” alisema Dkt. Naizihijwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Physiocare Tanzania, Remla Shirima, alisema wameshirikiana na kampuni ya Enovis ya Afrika Kusini katika kusaini makubaliano ya ushirikiano na JKCI kwa kuwatambua watu wanaojihusisha na michezo pamoja na kufanya mazoezi.
“Tunathamini kile kinachofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa wanamichezo, na kwa kutoa vifaa hivi vya fiziotherapia bila shaka vitaboresha na kusaidia huduma za utengamao kuwa bora na za kisasa zaidi,” alisema Remla.
Akizungumzia kuhusu ushirikiano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Enovis ya Afrika Kusini, Pieter Verwey, alisema wanathamini kile kinachofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete katika kuimarisha afya za wanamichezo kwa kuwafanyia uchunguzi kabla hawajaumwa anaamini vifaa hivyo vya teknolojia ya kisasa vitasaidia kuimarisha na kuboresha huduma za matibabu ya moyo hapa nchini.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Kampuni ya Physiocare Tanzania na Enovis ya Afrika Kusini wakiangalia utiwaji wa saini wa makubaliano ya ushirikiano wa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wanamichezo kupitia program ya Sports Cardiology uliokuwa unafanyywa na viongozi wa taasisi hizo leo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI
Naye, Mratibu wa Sports Cardiology kutoka JKCI Hospitali ya Dar Group Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo , Eva Wakuganda, alisema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni kwa muhimu kutokana na hatari iliyopo kwa wanamichezo ya kudondoka ghafla na kupoteza maisha wakati wanafanya mazoezi au wakati wa mashindano kutokana na mabadiliko yanayoweza kutokea ndani ya mioyo yao.
“Baadhi ya wanamichezo wamekuwa wakikumbana na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo au matatizo ya moyo ambayo hayajawahi kujulikana kwahiyo hatua hii ni muhimu sana katika kuboresha afya za wanamichezo,” alisema Dkt. Eva.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Kampuni ya Physiocare Tanzania na Enovis ya Afrika Kusini wakiangalia utiwaji wa saini wa makubaliano ya ushirikiano wa kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wanamichezo kupitia program ya Sports Cardiology uliokuwa unafanyywa na viongozi wa taasisi hizo leo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI
No comments