Dkt.Nchimbi atikisa Kanda ya Ziwa
Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi, akiwahutubia wananchi wa Bunda mkoani Mara leo Agosti 20,2025
Mwanza
MGOMBEA mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema chama hicho kitawafanyia mambo ya maendeleo wananchi wa Mkoa wa Mwanza, ikiwa watawapa ridhaa ya kuongoza kipindi cha miaka mitano ijayo.
Dkt.Nchimbi aliwashangaa watu wanaodai kuwa, chama hicho hakijafanya lolote, akibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Akihutubia wananchi wa Mwanza katika viwanja vya Furahisha, Dkt. Nchimbi amesema serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa katika sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barabara, huduma za maji na kijamii, hivyo wataendelea kutoa kipaumbelea kwenye miradi hiyo.
Amesema watahakikisha wanawasimamia na kuwawajibisha wabadhirifu wa mali za umma kwa manufaa ya watanzania wote.
Dkt.Nchimbi ametoa kauli hiyo Agosti 29,2025, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu iliyofanyika katika viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza, huku akiwanadi wagombea ubunge na udiwani mkoani humo.
Mgombea Mwenza huyo ameelezea yale ambayo serikali imeyatekeleza katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt.Samia madarakani, na yale watakayofanya ikiwa watanzania watawapa ridhaa kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29,2025.Dkt.Samia aliingia madarakani Machi 19,2021, akichukua nafasi ya Dkt.John Pombe Magufuli, aliyefarika Dunia Machi 17,2021
Amesema kuwa, serikali ijayo ya CCM itaendeleza kasi hiyo kwa kujenga zahanati mpya, vituo vya afya na kuhakikisha huduma za kibingwa zinapatikana katika hospitali za wilaya.
Pia, aliahidi miradi ya maji kufikia asilimia 90 ya upatikanaji, pembejeo nafuu kwa wakulima na barabara za lami ndani ya miaka mitano.
“Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kusema CCM haijafanya lolote. Ukiona mtu anasema hivyo haraka sana muwahishe hospitali,” amesema kwa msisitizo.
Mgombea mwenza huyo ametumia fursa hiyo kunadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 pamoja na kuwanadi wagombea wa chama hicho katika nafasi ya ubunge na udiwani ndani ya mkoa huo.
Akiwa mkoani Mara, Balozi Dkt.Nchimbi aliwanadi mgombea ubunge Jimbo la Bunda mjini, Easter Bulaya na wagombea udiwani wa jimbo hilo.
No comments