Maandalizi ZIFF yamekamilika
Kutoka kushoto; Mkurugenzi wa Goethe-Institut Tanzania Bw. Mpangi Otte, Mtendaji Mkuu wa ZIFF Joseph Mwale, Mkurugenzi wa ZIFF, Hatibu Madudu na Mwakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi, wakionesha nembo itakayotumika katika maonesho ya ZIFF mwaka huu.
Egbert Mtui
WAANDAAJI wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF), linalojulikana pia kama Tamasha la Nchi za Majahazi wamesema maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Juni 25 hadi 29 mwaka huu, Ngome Kongwe Zanzibar yamekalika.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Goethe-Institute Upanga jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale, akiwa na kamati ya maandalizi amesema maandalizi kwa ajili ya tamasha hilo lenye ujumbe unaosema ‘Tumaini linalochipukia’ yamekamilika kila idara.
“Kila kitu kimekamilika na leo mtapata orodha ya filamu pamoja na mataifa yatakayoshiriki tamasha hili ambalo limekuwa kivutio cha filamu nyingi kutoka nje na ndani ya nchi,” amesema Mwale.
Akizunguza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa ZIFF, Hatibu Madudu, amesema tamasha hilo litahusisha maonesho ya filamu, warsha, na panorama, kwamba mwaka huu wamepokea filamu 430 zilizotengenezwa kati ya mwaka 2024 na 2025 kutoka nchi mbalimbali duniani.
“Kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki tumepokea filamu 174, ambapo Kenya iliwasilisha filamu (54), Uganda filamu (52), Tanzania (49), Somalia nane (8), Rwanda 6, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nne (4), na Burundi filamu moja.
“Kadhalika tuna filamu kutoka India, Brazil, Marekani, China, Ufaransa , Italia, Uturuki, Nigeria, Argentina, Spain, Poland, United Kingdom, Germany, Canada, Indonesia, Russia Federation, Qatar, Japan, United Arab Emirates, Pakistan, Tunisia, Angola, Malawi, Portugal, Belgium, Zimbabwe, Mayote, Vietnam, Reunion, Romania, Saudi Arabia, Oman, Morocco, Lebanon, Jamaica, Botswana, Burkina Faso, Ghana, Senegal, Sudan na Ethiopia. Hizo ni baadhi ila tuna nchi zaidi 100,” amesema Madudu.
Mkurugenzi wa Goethe-Institut Tanzania Bw. Mpangi Otte alisema wanajivunia kudhamini tamasha hilo kubwa lenye hadhi ya kimataifa.
“ZIFF ni zaidi ya filamu, ni sauti, maono. Afrika inasimulia hadithi zake kwa ujasiri, uzuri wa aina yake. Goethe-Institut Tanzania, tunaamini utamaduni si ni jambo la muhimu sana. Hujuenga mijadala, mazungumzo, hujenga na kuchochea mabadiliko, ” amesema Bw Otte.
Wasanii ambao filamu zao zitaoneshwa katika tamasha hilo wameeleza furaha yao kupata fursa hiyo, huku wakitoa pongezi nyingi kwa waandaaji pamoja na wadhamini wa ZIFF mwaka huu.
Wadhamini wa ZIFF ni Umoja wa Ulaya (EU), Aza Media Ltd, Air Tanzania na CANNEX, Serikali ya Zanzibar, Wizara ya Utalii Zanzibar, Infinity Group Zanzibar, Maru Maru Hotel, Emerson Hotel, Goeth Institut, The Box, Archipelago Restaurant na Nafasi Film Club.
“Kwangu mimi naona nifahari kubwa sana kushiriki katika filamu na ikapata fursa ya kuoneshwa katika tamasha la ZIFF ambalo kwa aina yake ni kubwa sana, kwasababu linahusisha filamu kutoka mataifa mbalimbali,” amesema Tunu Mbegu aliyeshiriki katika filamu ya Niko Sawa iliyoongozwa na Neema Ndepanya.
Cecilia Lubango, mwongozaji wa filamu ya Tears in the Rain inayohusu afya ya akili, alisema kuwa ifike mahala fulani wasanii watumie filamu kuweka bayana matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii ya Watanzania.
“Kwanza ninafurahi kwamba filamu hii niliyoongoza mimi inakwenda kuoneshwa ZIFF. Hii ni mara ya kwanza kwangu, ila niwaombe wasanii wenzangu tutumie filamu kuanika matatizo katika jamii zetu,” alisema Lubango.
Katika hatua nyingine, Mwongoza filamu ya Ndoto Yangu, Sama Johanpow, inayohusu masuala ya elimu, amesema pamoja na kupata fursa filamu yake kuonesha katika tamasha la ZIFF yeye binafsi anajiona msanii wa filamu mkubwa katika miaka mitano ijayo.
“ZIFF ni jukwaa kubwa mno na hasa kwa watengeneza filamu kama sisi kupata fursa ya kuonekana filamu yako. Kwangu mimi, hii ni changamoto ili niweze kufanya vizuri zaidi, niwashukuru ZIFF kwa fursa hii,” amesema.
Filamu ya ufunguzi itakayooneshwa Juni 25 saa mbili usiku ni Janani The Last Stand kutoka Uganda iliyoongozwa na Matt Bish.
No comments