Header Ads

ad

Breaking News

Hazina yajivunia kuongeza mapato yasiyo ya kikodi

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akizungumza na wahariri, katika kikao kazi kilichofanyia jana jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

OFISI ya Msajili wa Hazina imerekodi ongezeko la asilimia 40 katika makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi ndani ya kipindi cha miezi 11, ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita.

Hayo yamebainishwa jana na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, kilichohusu mageuzi, mafanikio, mikakati na mwelekeo wa ofisi hiyo.

Alisema serikali imekusanya sh. bilioni 884.7 kuanzia Julai 2024 hadi Mei 2025.

Amefafanua kuwa, hilo ni ongezeko kubwa la mapato yanayokusanywa kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, ikilinganishwa na sh.bilioni 633.3 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2023/24.

“Hii inaonesha ongezeko la asilimia 15.3 ikilinganishwa na jumla ya makusanyo ya mwaka mzima ya sh. bilioni 767 katika mwaka wa fedha uliopita,”amesema.

Amefafanua kuwa, ukuaji huo wa mapato umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika mashirika ya umma na matumizi ya mifumo ya TEHAMA.

“Ofisi imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Mpango na Bajeti (PlanRep) na Mifumo ya ERMS na e-Watumishi, pamoja na kufanya maboresho ya Mfumo wa MUSE ambao unawezesha kupata taarifa halisi za matumizi katika Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma,” amesema Msajili wa Hazina.

Mchechu amesema maboresho hayo sasa yamefanya mifumo kubadilishana taarifa ipasavyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuona mifumo inasomana.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akizungumza 

Amevitaja vyanzo vikuu vya mapato kwa mwaka huu, ni gawio ambalo limechangia asilimia 63.9 ya mapato yote, huku michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ikichangia asilimia 29.7.

Aidha, mapato mengineyo yaliyojumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yamechangia asilimia 6.4 ya mapato yote.

Mbali na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato, pia uwekezaji katika kuimarisha utendaji wa watumishi wao kupitia viashiria muhimu vya utendaji (KPIs), umetajwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema kupitia KPIs, Ofisi hiyo imeweza kufanya tathmini za utendaji wa Bodi, ili taasisi ziwe na matokeo yanayopimika kwa uwazi na uwajibikaji.

“Hili limeenda sambamba na kuwajengea uwezo Viongozi wetu ambapo jumla ya Watendaji Wakuu 111 walishiriki mafunzo elekezi ya uongozi na usimamizi (CEO Induction) mwaka huu, ili kuimarisha utawala bora na uhusiano wa kiutendaji,” alisema Mchechu.

Hata hivyo, amesema ili kuongeza ufanisi zaidi na ukusanyaji wa mapato, serikali imeongeza uwekezaji wake katika mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.

Msajili wa Hazina amesema kwa sasa thamani ya uwekezaji wake imetoka sh. trilioni 75.79 mwaka 2022/23 hadi sh. trilioni 86.29 mwaka 2023/24.

“Tumeweza kuhamasisha uwajibikaji katika kampuni hizi kupitia Mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi wanaoiwakilisha serikali katika kampuni zenye hisa chache uliowaleta washiriki 125, na kuzindua mwongozo ulioboreshwa wa wakurugenzi,” amesema Msajili wa Hazina Mchechu.

Kwa mujibu wa msajili huyo, amesema hilo limeenda sambamba na kupitia mikataba na kuimarisha usimamizi wa hisa, huku ikiongeza ushiriki wake katika kampuni muhimu kwenye sekta za benki, viwanda na madini kupitia maboresho ya mikataba ya wanahisa na miundo ya usimamizi.

Malengo ya makusanyo

Amesema ofisi yake ina shauku ya kukusanya sh. trilioni 1 kama mapato yasiyo ya kodi katika mwaka huu wa fedha wa 2024/25.

Amefafanua kuwa, tayari karibu sh. bilioni 900 zimekusanywa kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache zipatazo 200.

“Hadi kufikia sasa Juni 2, 2025, Ofisi ya Msajili wa Hazina imekusanya karibu sh. bilioni 900 kama mapato yasiyo ya kodi, na matamanio yetu ni kukusanya sh. trilioni1 katika Mwaka wa Fedha wa 2024/25,” amesema Mchechu.

Aidha, ikiwa ofisi hiyo itafanikiwa kukusanya sh. trilioni 1, itakuwa ni ongezeko la asilimia 30.4 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita, ambapo kiasi cha sh bilioni 767 zilikusanywa.

Ili kuhakikisha ofisi hiyo inafikia adhma hiyo ya kukusanya sh. trilioni 1, Msajili wa Hazina amezitaka taasisi ambazo hazijawasilisha gawio, zifanye hivyo ndani ya wiki hii.

“Taasisi zote ambazo bado hazijawasilisha gawio kwa serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, zinapaswa kufanya hivyo ndani ya wiki hii, ili ifikapo siku ya gawio, Juni 10 mwaka huu, asiwepo wa kudaiwa,” amesema Mchechu.

Mchechu amesema ukuaji wa mapato yasiyo ya kodi umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika mashirika ya umma na matumizi ya mifumo ya TEHAMA.

Kuhusu siku ya gawio

Akizungumzia siku ya gawio 2025, Mchechu alisema inatarajiwa kufanyika Juni 10, mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema katika siku hiyo, taasisi na mashirika ya umma yatamkabidhi rasmi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, michango na gawio kwa serikali.

“Tukio hili ni muhimu sana si tu kama alama ya uwajibikaji, bali kama chombo cha kutathmini utendaji wa mashirika na taasisi za umma kwa mujibu wa malengo ya taifa,” amesema Mchechu.

Amesema siku ya gawio imekuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi na mafanikio yanayooneka leo kwani, tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu wa wazi na wenye uwajibikaji, kumekuwa na ongezeko la mashirika yanayotoa gawio, pamoja na kuboreshwa kwa utendaji wao kwa ujumla.   

“Hii ni ishara kuwa pale ambapo taasisi za umma zinasimamiwa kwa weledi, mafanikio ya kweli yanawezekana,” amesema Mchechu.

No comments