WAZIRI MAVUNDE AZINDUA TAARIFA YA UCHAMBUZI UONGEZAJI THAMANI MADINI MUHIMU TANZANIA
* Asema Tanzania imeanza safari ya mageuzi sekta ya madini
*Asisitiza dhamira ya Tanzania kuwa kitovu cha bidhaa zitokanazo na madini muhimu.
*Balozi wa Uingereza nchini asema hatua hiyo ni kielelezo cha ushirikiano
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde ameeleza kuwa, serikali imeendelea kuchukuwa hatua madhubuti kuelekea mageuzi ya kweli ya sekta ya madini nchini, kwa kuanza rasmi mkakati wa kuongeza thamani ya madini muhimu yanayopatikana nchini.
Ameeleza hayo Mei 8, 2025 wakati akizindua rasmi taarifa ya uchambuzi wa kina wa uongezaji thamani madini muhimu na mkakati ya Tanzania (Manufacturing Africa – Critical Minerals Value Addition Study), katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young akiongozana na maafisa wandamizi wa Ubalozi huo, wadau wa sekta ya madini, wawekezaji, na wawakilishi, Waziri Mavunde amesema utafiti huo ni hatua muhimu katika kufanikisha azma ya taifa ya kuyachakata madini muhimu na mkakati ndani ya nchi hadi kufikia bidhaa za mwisho kwa matumizi ya ndani na nje.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini muhimu kama vile nickel, graphite, rare earth elements na lithium, madini ambayo ni mhimili wa teknolojia za kisasa, magari ya umeme na nishati mbadala duniani.
“Kwa kuwekeza katika uongezaji thamani wa madini haya, tunajipanga kuwa kitovu cha uzalishaji wa malighafi ya kisasa kwa ajili ya soko la kimataifa,” amesisitiza Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, serikali imeweka mazingira rafiki kwa uwekezaji kwa kuboresha miundombinu, kujenga uwezo wa kitaalamu, na kuweka sera na motisha zinazowezesha uwekezaji katika mitambo ya uchenjuaji, uchenjuzi, na uzalishaji wa bidhaa za mwisho.
“Utafiti huu utaisaidia serikali kutambua maeneo mahsusi ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini, pamoja na fursa mpya za kiuchumi zitakazochochea maendeleo hapa nchini,” ameongeza Mavunde.
Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini Marianne Young, amesema taarifa hiyo ni sehemu ya ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya sekta ya madini, na Wamba mkakati wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini ya Uingereza kushirikiana na GST kubadilishana uzoefu katika eneo la utafiti wa kina wa madini.
Uchambuzi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa ushirikiano wa kimkakati wa ushirikiano wa stawi wa pamoja kati ya Tanzania na Uingereza uliozinduliwa mwaka jana.
Mpango huo pia unalenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kwenye sekta ya viwanda, hasa kwa kutumia madini muhimu/mkakati kama malighafi ya msingi.
.Waziri wa Madini Anthony Mavunde (kulia), na Balozi wa Uingereza nchini, Marianne Young akiwa katika picha ya pamoja
No comments