Header Ads

ad

Breaking News

PURA yawabana wawekezaji ikitetea mgawo wa Tanzania fedha za gesi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni akiwasilisha wasilisho lake katika kikao na wahariri wa habari jana jijini Dar es Salaam

*Ukaguzi waokoa Sh bilioni 340 za mgawo zilizokuwa 'zimepotea'

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imefafanua namna inavyodhibiti uwekezaji katika utafutaji wa rasilimali za gesi na mafuta, ili ugunduzi unapopatikana Tanzania ipate mgawo stahiki wa faida ya biashara ya rasilimali hizo.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, alisema wawekezaji wanaotafuta rasilimali hizo wakija nchini, hutakiwa kutumia fedha zao katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia na wakikosa hurudisha eneo walilokabidhiwa kwa Serikali na kuondoka. 

"Pindi mwekezaji akigundua mafuta au gesi asilia, fedha zitakazopatikana baada ya mauzo ya rasilimali iliyopatikana, zitalipa mrabaha, zitarudisha mtaji aliowekezwa wakati wa utafutaji, hulipa kodi na tozo mbalimbali na kinachobaki hugawiwa kwa wabia wa mkataba, ikiwemo Serikali na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)," alisema Sangweni.

Kutokana na jukumu hilo, Sangweni amesema PURA imeendelea kuhakiki na kukagua mapato na gharama za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji katika Mikataba ya Ugawanaji

Mapato kati ya Serikali na Waendeshaji wa Vitalu (PSA Auditing), ili kuhakikisha Serikali inapata mgawo stahiki kwenye mapato ya mafuta na gesi asilia.

Sangweni akizungumzia miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema PURA hufanya uhakiki na ukaguzi wa kiasi wa fedha zinazowekezwa pamoja na shughuli zinazotekelezwa, ili kuepuka udanganyifu unaoweza kufanywa na mwekezaji, wakati wa kurejesha mtaji alioutumia katika utafutaji.

Amesema kupitia kaguzi hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 340 zimerejeshwa kwenye Mfuko wa Ugawanaji wa Mapato Kati ya Serikali na Wawekezaji katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, ambapo fedha hizo zingeweza kutumika kama marejesho ya mtaji wa mwekezaji, kama uhakiki wa PURA usingezibaini kuwa ni fedha za ugawanaji faida.

Alisema katika miaka hiyo minne, Serikali imetoa leseni ya uendelezaji katika eneo la ugunduzi la Ntorya mkoani  Mtwara na kufanya ukarabati wa visima vitano ambao umechangia uimara wa uzalishaji wa gesi asilia.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina SAbato Kosuri akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kilichoratibiwa na ofisi yake

Mafanikio mengine aliyotaja ni pamoja na kuimarika kwa shughuli za uhakiki na kaguzi za mikataba ya uzalishaji na ugawanaji wa mapato, ongezeko la shughuli za wazawa katika mkondo wa juu wa petroli na kuimarika kwa kampuni za kizawa kuingia ubia na kampuni za kigeni, katika kutoa huduma za teknolojia na utaalamu wa kina katika shughuli za mafuta na gesi.

Mhandisi Sangweni alisema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa matumizi na ufungamanishaji wa mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa shughuli za mafuta na gesi, kuimarika kwa Kampuni ya Taifa ya Mafuta (TPDC), katika uchukuaji wa data za mitetemo pamoja na kuwezesha tafiti za awali za kijiolojia, kijiofizikia na kijiokemia katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

"Kuimarika kwa ushirikiano kati ya PURA na taasisi za kiudhibiti za nishati katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na kuimarishwa kwa mfumo wa udhibiti kwa kuandaa na kuboresha kanuni na miongozo mbalimbali ya kisheria," alisema.

Mkurugenzi Mkuu huyo ameendelea kutaja mafanikio mengine kuwa ni, kuendelezwa kwa majadiliano ya uwekezaji katika mradi mkubwa wa kuchakata na kusindika gesi kuwa katika hali ya kimiminika na kuongezeka kwa watumishi 48 kutoka idadi ya 45 mwaka 2021 hadi kufikia watumishi 93 mwaka 2025 ambapo imeimarisha ufanisi katika usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu. 

Mhandisi Sangweni ameongeza kuwa, kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2025, kiasi cha gesi asilia kilichozalishwa kimefikia Futi za Ujazo bilioni 301.33. 

Amesema kati ya kiasi hicho, Futi za Ujazo bilioni 142.35 zilizalishwa kutoka Kitalu cha Mnazi Bay na Futi za Ujazo bilioni 158.98 kutoka Kitalu cha Songo Songo, ambapo uzalishaji huo ni wastani wa Futi za Ujazo bilioni 35.59 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na Futi za Ujazo bilioni 39.74 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo. 

Afisa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Majili wa Hazina, Alex Malanga akiongoza kikao kazi

Sangweni amesema katika kipindi cha nyuma, uzalishaji wa gesi ulikuwa wastani wa Futi za Ujazo bilioni 32.03 kwa mwaka kwa upande wa Mnazi Bay na Futi za Ujazo bilioni 25.13 kwa mwaka kwa upande wa Songo Songo.

"Gesi asilia iliyozalishwa ilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani, majumbani, taasisi na katika magari," amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.

Amesema majukumu ya msingi ya PURA, ni kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa mafuta na gesi, ambapo PURA hufanya mapitio na kuidhinisha mpango kazi na bajeti za kila mwekezaji inapofika mwanzo wa mwaka. 

Katika mwaka husika, PURA huendelea kufanya usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ambayo yameidhinishwa katika mpango kazi na bajeti ya mwaka huo.

Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Tausi Caren Mbowe wakisikiliza maswali

 Mhandisi huyo amesema masuala mengine muhimu ambayo PURA husimamia ni uhusishwaji wa wazawa na makampuni ya kizawa kwenye shughuli hizo.

"PURA tunahakikisha utekelezaji wa shughuli hizo unaendana na thamani ya fedha zilizoidhinishwa kwa kufanya kaguzi za hesabu na matumizi ya kila mkataba," amesema Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Sangweni.

Uwekezaji katika tasnia hiyo hufanyika kupitia vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi ambavyo vipo maeneo ya baharini na nchi kavu, vitalu hivyo vimegawanywa kwa kuzingatia tafiti za awali ambazo zimekuwa zikifanywa na wataalamu kutoka PURA. 

"Pale inapoonekana kuna viasiria vya uwepo wa mafuta katika eneo fulani ndipo eneo hilo hugawanywa kuwa vitalu. Vitalu hivi hunadiwa kwa njia ya ushindani ili kupata wawekezaji ambao kwa mujibu wa sheria huingia mikataba ya PSA na Serikali, ambapo hadi sasa Tanzania imefanya duru za kunadi vitalu zipatazo nne, ambapo ya mwisho ilifanyika mwaka 2013."

"Kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia huongeza uwekezaji katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini. Uwekezaji huu husaidia kuongezeka kwa shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia hivyo kusababisha ugunduzi zaidi wa gesi asilia na mafuta. 

Mhariri wa Raia Mzalendo, Joseph Mwendapole akiuliza swali

"Faida za kunadi vitalu, ni pamoja na kuongezeka kwa ugunduzi na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini, kukua kwa uchumi wa nchi kutokana na mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia na kuwezesha upatikanaji wa 'data' za petroli utakaoongeza wigo wa taarifa zitakazosaidia katika kuchochea utafutaji zaidi wa mafuta na gesi asilia nchini."

"Kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania na matumizi ya bidhaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara na watoa huduma wa kitanzania," amesema.

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, Mhandisi Sangweni amesema PURA imeendelea kusimamia matakwa ya sheria kuhusu ushiriki wa Watanzania na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanaotoa huduma wananufaika na fursa zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia.

"Kupitia usimamizi makini, ushiriki wa Watanzania katika ajira umekuwa wa wastani wa asilimia 85 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ambapo ushiriki wa Watanzania ulikuwa chini ya asilimia 50.

"Aidha, manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani imekuwa katika wastani wa asilimia 60 kwa bidhaa na huduma za ndani ikilinganishwa na asilimia chini ya 40 kwa miaka ya nyuma," amesema.

Mhariri wa Blog ya Fullshangwe, John Bukuku akiuliza swali katika kikao kazi

Sambamba na hilo, PURA imeendelea kusajili watoa huduma wa kitanzania na Watanzania waliosomea masuala ya mafuta na gesi asilia katika kanzi data ijulikanayo kama Common Qualification System (CQS).

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) iliundwa kupitia Kifungu Na. 11 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015. Kwa

mujibu wa Sheria hiyo, PURA ina majukumu ya kuishauri Serikali na Waziri mwenye dhamana ya nishati kuhusu masuala ya mkondo wa juu wa petroli.

Majukumu mengine pamoja na kudhibiti na kusimamia shughuli za mkondo wa juu wa petroli, na kudhibiti na kusimamia shughuli za uchakataji na usindikaji wa gesi asilia kuwa kimiminika (Liquefied Natural Gas - LNG).

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wariri tanzania (TEF), Anitha Mendoza, akifuatilia wasilisho
Wahariri na maafisa wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wakisikiliza wasilisho kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo
Wahariri na maafisa wa PURA wakifuatilia wasilisho katika kikao kazi kilichofanyika jana


No comments