Prof. Janabi achaguliwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika
Mshauri wa Rais wa Masuala ya Tiba nchini Tanzania na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi
MSHAURI wa Rais wa Masuala ya Tiba nchini Tanzania na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika katika uchaguzi uliofanyika leo, Mei 18, 2025, jijini Geneva, Uswisi.
Prof. Janabi alikuwa mgombea pekee kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, akiwania nafasi hiyo dhidi ya wagombea wanne kutoka Afrika Magharibi. Wagombea hao ni Dkt. N’da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dkt. Dramé Mohammed Lamine (Guinea), Dkt. Boureima Hama Sambo (Niger), na Prof. Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.
Katika kampeni yake ya kuwania nafasi hiyo, Prof. Janabi aliwasilisha vipaumbele saba mbele ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa WHO barani Afrika, akisisitiza umuhimu wa maboresho ya huduma za afya, upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya kugharamia huduma bora, na maandalizi ya kukabiliana na majanga na dharura za kiafya.
Uchaguzi huo umefanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, aliyefariki dunia kabla ya kuanza rasmi majukumu yake.
No comments