JKCI kuwafanyia uchunguzi wa moyo wateja wa ATC
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na viongozi kutoka Shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) wakati wa kikao cha kuangalia namna ambavyo watashirikiana kutoa huduma kwa wateja wanaotumia shirika hilo kupata huduma za uchunguzi wa afya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Na Mwandishi maalumu, Dar es Salaam
WATEJA wanaotumia ndege ya Air Tanzania kupata ofa ya kufanya uchunguzi wa afya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Ofa hiyo itatolewa kwa wateja wanaokata tiketi daraja la biashara (Business) kwa safari za ndani ya nchi na daraja la biashara na uchumi (Business and Economy) kwa safari za nje ya nchi.
Akizungumza mara baada ya kufanya kikao na viongozi kutoka shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imeona fursa ya kushirikiana na shirika hilo kama sehemu ya kuimarisha tiba utalii nchini.
“Ndege ya Shirika la Air Tanzania sasa inasafiri nchi mbalimbali Afrika na nje ya Afrika, tukitumia fursa hii kutoa ofa ya uchunguzi wa afya kwa wateja wake tutakuza utalii tiba nchini”, alisema Dkt. Kisenge.
Meneja masoko wa Shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) Christina Tungalaza akifafanua jambo wakati wa kikao cha kujadili namna shirika hilo linaenda kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa huduma za uchunguzi wa afya kwa wateja wake jana jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema JKCI na ATCL wapo katika mkakati wa kuidhinisha makubaliano ya ushirikiano huo ambao utalifanya Shirika hilo kuwa la kwanza kuwezesha huduma za uchunguzi wa afya kwa wateja wake nchini.
“Wateja wa Air Tanzania sasa wajiandae kupata huduma bingwa na bobezi za uchunguzi wa afya katika Taasisi yetu, tunawahaidi mkitibiwa kwetu hamtaenda hospitali nyingine,” alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Meneja Masoko kutoka Shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL), Christina Tungalaza alisema ushirikiano na JKCI utasaidia kuongeza wateja wanaotumia ndege hiyo na kuongeza pato la Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akisalimiana na viongozi kutoka Shirika la ndege la Air Tanzania alipotembelea shirika hilo jana kujadili namna ambavyo watashirikiana kutoa huduma za uchunguzi wa afya kwa wateja wanaotumia ndege ya ATCL.
Christina alisema mbali na kuongeza wateja wanaotumia ndege hiyo ushirikiano huo utasaidia kupunguza wagonjwa wanaoenda nje ya nchi kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya kwa kutumia fursa hiyo kuchunguza afya zao JKCI.
“Tumekuwa tukipata wateja wanaotumia ndege yetu kwenda nje ya nchi kwaajili ya kufanya uchunguzi na matibabu, tukianza ushirikiano na JKCI itawapunguzia wateja wetu adha ya kufuata huduma za afya nje ya chini na kutibiwa hapa nchini,” alisema Christina.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) mara baada ya kumalizika kwa kikao cha mashirikiano kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam. Picha na: JKCI
No comments