TFS Lindi yagawa miche 300 ya matunda na mbao
KATIKA kuadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Ofisi ya Mkoa wa Lindi, imeshiriki kikamilifu katika sherehe hizo kwa kugawa miche 300 ya miti ya mbao, matunda na kivuli kwa wananchi.
Shughuli hiyo imefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nyengedi, iliyopo katika Halmashauri ya Mtama, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mheshimiwa Victoria Mwanziva, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo mapema leo, Mheshimiwa Mwanziva aliipongeza TFS kwa juhudi kubwa katika kuhifadhi mazingira kupitia upandaji wa miti, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu muhimu ya kutunza rasilimali za taifa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Tuna kila sababu ya kuunga mkono juhudi hizi, kwani miti inabeba uhai wa Taifa letu. Tuipokee na kuitunza miche hii ili iwe urithi wa kizazi kijacho. Zoezi hili pia linaunga mkono kaulimbiu ya kitaifa kuhusu lishe bora kupitia upandaji wa miche ya matunda, hivyo kusaidia kuboresha afya za wananchi wetu,” alisema Mwanziva.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Rondo, PCO John Olomi, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TFS katika juhudi za kulinda mazingira, huku akieleza utaratibu wa upatikanaji wa miche kutoka kwa Wakala huo.
“TFS itaendelea kutoa elimu ya mazingira na kuhamasisha upandaji wa miti kwa maendeleo endelevu. Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea bustani zetu za miche na kujipatia miche bure kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo yao binafsi, mashamba madogo, shule na taasisi mbalimbali,” alisema Olomi.
Aidha, alifafanua kuwa, “Kwa wakulima na wananchi wa kawaida, miche ya miti hutolewa bila malipo. Hata hivyo, kwa wale wanaohitaji miche kwa ajili ya mashamba ya miti ya kibiashara, mche mmoja huuza kwa bei ya serikali ya Shilingi 500 hadi 600.”
Akibainisha zaidi utaratibu wa maombi, Mhifadhi Olomi alisema kuwa, “Mahitaji ya miche kwa mwananchi mmoja mmoja hutumwa kwa kupitia uongozi wa vijiji vyao, ambao hufanya majumuisho ya maombi yote na kuyawasilisha kwa Meneja wa Wilaya au Meneja wa Shamba husika. Utaratibu huu umewekwa mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji sahihi wa taarifa na ufuatiliaji wa matumizi ya miche inayotolewa.”
“Tunawakaribisha wote kutumia fursa hii kuanzisha mashamba au bustani za miti, kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato kupitia kilimo cha miti na mazao ya matunda,” alisisitiza Mhifadhi Olomi.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa:“Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” ikisisitiza mshikamano, amani na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.
TFS inaendelea kuhamasisha wananchi kuwa sehemu ya juhudi za kitaifa za kulinda na kuhifadhi misitu na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
No comments