RC Malima aongoza zoezi la VOTENOW mkoani Morogoro, watanzania waitikia wito
Na Zainab Ally, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, amepongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa ubunifu wa kuandaa kampeni za kuhamasisha upigaji kura kupitia mpango wa VoteNow unaolenga kuzipatia ushindi hifadhi za Tanzania katika tuzo za kimataifa za World Travel Awards 2025.
Akizungumza leo Aprili 26, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Malima amesema kampeni hizo siyo tu zinawapa watanzania elimu juu ya umuhimu wa uhifadhi, bali pia zinawachochea kuonesha uzalendo kwa kushiriki kupigia kura maeneo ya asili yanayoiwakilisha Tanzania duniani.
Amebainisha kuwa ushindi katika tuzo hizo ni hatua muhimu katika kutangaza utalii na kuhifadhi hadhi ya taifa kimataifa.
Kwa upande mwingine, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki anayesimamia Kitengo cha Biashara na Masoko, Fredrick Malisa, ameongoza zoezi hilo kwa kushirikiana na timu ya hamasa kutoka TANAPA.
Akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Malisa amesema kampeni ya VoteNow inaendelea vizuri nchi nzima huku ikipokelewa kwa mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi mbalimbali waliotambua nafasi yao katika kulinda na kutangaza urithi wa taifa.
Malisa ameongeza kuwa, mbinu mbalimbali zimetumika kuwafikia watanzania wengi, ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara, kuendesha vipindi maalum kwenye redio na televisheni na kushirikiana na viongozi wa kijamii na dini.
Amesema kuwa, ni pamoja na kufanya kampeni za moja kwa moja kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ili kuwahamasisha wanafunzi kupiga kura na kuwa mabalozi wa utalii. Pia, mitandao ya kijamii imetumika kwa kasi kueneza ujumbe wa kampeni hiyo kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Malima amehitimisha kwa kuwasihi Watanzania wote kuendelea kushiriki kwa wingi katika kampeni ya VoteNow kwa kuwa kila kura ni mchango mkubwa kwa taifa.
Amesema ushindi wa hifadhi za Tanzania katika World Travel Awards 2025 utakuwa ushindi wa kila Mtanzania na wa taifa zima katika kulinda na kutangaza urithi wa asili.
No comments