Header Ads

ad

Breaking News

Wasanii wa filamu wapongezwa kuutangaza utalii

Na Joyce Ndunguru, Dar es Salaam

UMOJA wa Waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam umepongezwa kwa kubeba maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii.

Maneno haya yalisemwa Novemba 2,2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe.Saad Mtambule katika tamasha la "Shtuka, Boresha Afya ya Akili ndani ya Hifadhi ya Pande" lililoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kwa kushirikiana na Umoja wa Waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam.

"Niwapongeze wasanii wa sekta ya uigizaji kwa kubeba maono ya Rais Dkt.Samia ya kuitangaza sekta ya utalii na hasa, Hifadhi yetu ya Pande ambayo inapatikana kwenye Wilaya yetu ya Kinondoni," alisema Mhe.Mtambule.

"Pia, tuendelee kutumia akaunti zetu za mitandao ya kijamii kuhamasisha makundi mbalimbali ili yaweze kuja kutembelea hifadhi ya Pande," aliongeza Mhe.Mtambule.

Mhe.Mtambule, aliwashukuru wasanii kwa kutembelea hifadhi hiyo na alisisitiza kuwa, utangazaji wa shughuli za utalii ukiongezeka wageni watafurika hivyo, uchumi wa nchi utakua.

Mkuu wa wilaya huyo ameipongeza TAWA kwa jitihada zake za kuboresha Hifadhi ya Pande kwa kuongeza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo uanzishwaji wa bustani ya wanyamapori mbalimbali wakiwemo simba,duma, chatu, mamba, nyumbu na pundamilia.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, William Kitebi akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TAWA, alitoa shukrani zake za dhati kwa Mhe.Mtambule kwa ushirikiano wake na TAWA katika masuala ya uhifadhi wa Hifadhi za Pande na Kunduchi. 

Aliushukuru Umoja wa waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam kwa kutembelea Hifadhi ya Pande.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.Leonard Mwinuka alisema wao kama wasanii wataendelea kumuunga mkono Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika utangazaji wa utalii.

Pia, aliushukuru uongozi wa TAWA kupitia Hifadhi ya Pande kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha, "Mbegu mliyopanda kwetu, itaota na tutakuwa mabalozi wazuri wa kuelezea uzuri wa hifadhi hii,"alisisitiza, Bw.Mwinuka.

Tamasha hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa TAWA pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wakiwemo Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia Huduma za Biashara, Hamza Hassani, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sylvester Mushy, Mkurugenzi wa Masoko kutoka TTB, Ernest Mwamaja na Kamanda wa Pori la Akiba Pande, Dorothea Massawe.

Sambamba na hilo, tamasha hili liliambatana na zoezi la uchangiaji wa damu salama.









No comments