Tume ya Madini yaweka dharani mafanikio, yachangia asilimia 10 ya Pato la Taifa
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo
Na Mwandishi Wetu
TUME ya Madini imesema kutokana na mikakati iliyojiwekea hadi mwisho wa mwaka wa
fedha 2024/2025 itakuwa imeweza kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa kutoka asilimia 9 ya sasa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari, leo Oktoba 24, 2024 katika ukumbi wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Lwamo amesema lengo hilo linaendana na juhudi za kuongeza makusanyo ambapo katika mwaka huu wa fedha wamejiwekea lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Tume ya Madini imepata mafanikio makubwa, ikiwemo ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli, kuongezeka kwa usimamizi kwenye biashara ya madini na ukaguzi wa migodi na mazingira sambamba na ushirikishwaji wa watanzania katika sekta hiyo.
Amesema kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini, kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu.
Aidha, Mhandisi Lwamo ameweka wazi uelekeo wa Sekta ya Madini katika kuchangia Pato la Taifa ili kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango Mkakati wa Tume ya Madini wa Mwaka 2024/2025, 2025/2026.
Mhandisi Lwamo anasema, Tume ya Madini imeweka mikakati endelevu ikiwemo kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs), vitendea kazi (PoS) pamoja na kushirikisha Mamlaka nyingine za Serikali.
Lwamo amesema watashirikiana na (Halmashauri, Polisi, TARURA na TANROADS) na kuongeza kuwa, lengo ni kuongezeka kwa makusanyo yatokanayo na rasilimali ya madini ujenzi na madini ya viwandani.
Ametaja mkakati mwingine ni kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususani utoroshaji wa madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia Masoko na vituo vya madini nchini; kuimarisha vituo vya ukaguzi (exit-points) katika maeneo ya mipakani, bandarini pamoja na viwanja vya ndege lengo likiwa ni kupunguza matukio ya utoroshaji wa madini na hivyo kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na mapato stahiki.
“Uboreshaji na usimamizi thabiti wa Mfumo wa Utoaji wa Leseni za madini, matokeo ni kupunguza migogoro itokanayo na mwingiliano wa maombi ya leseni, kupunguza muda wa utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya leseni zitakazotolewa kwa mwaka hivyo kuhamasisha uwekezaji,”anasema Mhandisi Lwamo.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo anasema wamejipanga kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira, lengo kuongeza mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu unaojali mazingira kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
“Tutaimarisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs) na Maabara katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wadau hivyo kuchochea uwekezaji utakaowezesha Serikali kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini,” anasema.
Ametaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za tafiti zinazohusiana na utambuzi wa vyanzo vipya vya mapato yatokanayo na rasilimali za madini, lengo likiwa ni kuiwezesha Taasisi kuongeza wigo wa makusanyo yatokanayo na rasilimali madini ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa wachimbaji wa madini ili kuongeza mapato, ajira na kuwa Sekta endelevu.
Mhandisi Lwamo anasema vilevile, ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023 kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta, Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa utaongezeka na kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
"Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunakuwa moja ya taasisi yenye mchango mkubwa kwenye pato la taifa, tunaona tunaenda vizuri kwani kwa sasa makusanyo yanaongezeka," anasema.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo tulipewa lengo la kukusanya shilingi Trilioni Moja, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka.
Amesema, wizara, Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini iliendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa Madini nchini.
Kwa upande mwingine Mhandisi Lwamo katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 mauzo ya madini katika masoko na vituo vya ununuzi wa madini yalikua Shilingi trilioni 2.592.02 na mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo hayo ni kiasi cha shilingi bilioni 180.13 ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2021/2022 ambapo ilikua shilingi trilioni 2.361.80 na mapato ya Serikali yaliyopatikana ni Shilingi bilioni 164.09 ambapo mapato hayo yalihusisha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini.
Anasema, Tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.
Mhandisi Lwamo amesema, katika kipindi rejewa, jumla ya Mipango 1,050 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,036 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 14 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho.
“Aidha Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Makampuni mbalimbali ya Uchimbaji ambapo katika kipindi rejewa Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,356 ambapo kati ya hizo 18,853 ni Watanzania sawa na asilimia 97.40 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.60 ya ajira zote zilizozalishwa,”anasema Mhandisi Lwamo.
Vilevile, amesema jumla ya bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.780 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo kampuni za watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.46 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.
Amesema leseni hizo zilijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini.
Vilevile, Tume imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Madini nchini kwa kutoa leseni kubwa kwa makampuni mbalimbali ya uchimbaji wa madini.
"Leseni hizo za uchimbaji mkubwa wa Madini zilitolewa kwa Faru Graphite Corporation Limited itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya kinywe Wilayani Mahenge yenye leseni SML- 676/2022; Mamba Minerals Corporation Limited inayojihusisha na uchimbaji wa Rare Earth Elements-REE katika eneo la Ngualla yenye leseni SML 693/2022 iliyopo mkoani Songwe."
Pia, leseni ya usafishaji madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera yenye leseni SM- 651/2021; na Sotta Mining Corporation Limited iliyopo mkoani Mwanza, Wilaya ya Sengerema yenye leseni SML-653/2021," anasema.
Anasema, utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa katika Sekta ya Madini pamoja na sekta fungamanishi nchini ikiwemo Tume kuendelea kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa.
Pia, kufanya ukaguzi katika ujenzi na matumizi salama ya mabwawa ya topesumu (TSF) pamoja na uhifadhi wa miambataka (WRD). Katika kipindi kinachorejewa, Tume ya Madini ilifanikiwa kufanya kaguzi katika migodi mikubwa tisa ya uchimbaji wa madini iliyopangwa kukaguliwa katika Mikoa sita ya kimadini ambayo ni Mara, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita na Mtwara; sambamba na kufanya kaguzi 144 katika migodi ya kati nchini.
Pia, katika kipindi rejewa, Tume imefanikiwa kufanya ukaguzi katika masuala ya usalama, afya, mazingira katika migodi midogo 47,535 iliyopo katika Mikoa ya kimadini ya Morogoro, Tabora, Arusha, Kahama, Mwanza, Tanga, Manyara, Iringa, Njombe, Mbogwe, Shinyanga, Dodoma, Kigoma, Kagera, Chunya, Geita, Mara, Mbeya, Rukwa, Lindi, Ruvuma, Mtwara, Songwe, Pwani, Dar es Salaam na Katavi kwa uchache.
“Mafunzo kuhusu masuala ya usalama, afya, mazingira pamoja na usimamizi wa baruti yalitolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini katika Mikoa mbalimbali ya kimadini nchini ambapo jumla ya wachimbaji wa Madini 10,385 walishiriki mafunzo hayo,”anasema Mhandisi Lwamo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Lwamo ameipongeza Wizara ya Madini chini ya Waziri wake, Anthony Mavunde kwa kuiwezesha Tume ya Madini kupata bajeti ya kutosha ikiwa ni pamoja na vifaa kama vile magari, mashine za kupima madini ya metali na kuongeza bajeti.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jane Mihanji akitoa neno la shukrani
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEFF) Jane Mihanji, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa jukwaa hilo Deodatus Balile, amesema Sekta ya Madini imepiga hatua ukilinganishwa na kipindi cha nyuma.
“Tunatamani kuona Tume inaendelea kudhibiti Sekta ya Madini kupitia usimamizi ufuatiliaji na udhibiti wa utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini kwa ajili ya maendeleo endelevu ili kila mtanzania afaidike na rasilimali hii muhimu ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa,”amesema Mihanji.
Anasema ni vyema kukawa na mikutano ya mara kwa mara na wahariri kwani vyombo vya habari vimekuwa ni kiungo muhimu cha mawasiliano katika kuhabarisha umma.
Maafisa wa Tume ya Madini, wahariri na waandishi wa habari
Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza wasilisho
Wahariri na waandishi wa habari wakiwa makini wakisikiliza wasilisho
No comments