Header Ads

ad

Breaking News

Watu 335 wapata huduma za upimaji na matibabu ya moyo Dar es Salaam

Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)Hospitali ya Dar Group Jane Mathew akimpima kiwango cha sukari kwenye damumtoto aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi namatibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dares Salaam.

Na Stela Gama, Dar es Salaam

WATU 335 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwenye  kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili  iliyomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI, Hospitali ya Dar Group.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dkt.Tulizo Shemu, amesema matibabu hayo ya tiba mkoba yajulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services yamefanyika maalumu kwa ajili ya kusogeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Dkt. Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, amesema katika kambi hiyo, watu waliowaona walitoka ndani na nje ya Dar es Salaam na wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na matatizo mengine ya moyo.

“Nusu ya watu tuliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na wengine walikuwa na matatizo ya kutanuka kwa moyo, mishipa ya damu ya moyo kuziba, mafuta mengi kwenye mishipa ya damu, maumivu ya kifua, shida za valvu, shida ya mfumo wa umeme wa moyo.

"Pia, tumewaona watoto waliokuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa kwenye mpangilio wake.”

“Tuliowakuta na shida za moyo na wengine waliokuwa na shida mbalimbali za mwili kama vile masikio, mifupa, ngozi, macho tumewapeleka katika kliniki zetu kwa ajili ya matibabu kwani, katika hospitali hii licha ya kutibu moyo tunatibu pia magonjwa mengine pia wengine tumewapa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),” amesema Dkt.Shemu.

Dkt.Shemu amesema kambi za aina hiyo zitakuwa zikifanyika mara kwa mara katika hospitali hiyo kwani, kwa kufanya hivyo wananchi wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani watafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Kwa upande wa wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo wameishukuru Serikali kwa huduma waliyopata na kuomba iwe endelevu ili watu wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Tatu Hassan, mkazi wa Shinganya alisema aliona katika TV tangazo la kufanyika kwa matibabu hayo na kuchukuwa hatua ya kwenda kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Ninaishukuru Serikali kwa kutuangalia wananchi wanyonge wenye kipato cha chini na kutufikishia huduma hii ya matibabu ya kibingwa. Nimefika hapa nimefanyiwa vipimo, nimepewa ushauri na dawa za kwenda kutumia mwezi mmoja kwani, nina tatizo la shinikizo la juu la damu ambalo limesababisha moyo wangu kutanuka,” amesema Tatu.

“Ninatoa wito kwa wananchi wenzangu wanapoona matangazo ya upimaji wa magonjwa mbalimbali wasipuuze, wawahi hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu mapema kuliko kusubiri hadi waumwe ndipo waende kutibiwa,” amesema Richard John, mkazi wa Tegeta.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo kwa kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali nchini. 

Hadi sasa wametoa huduma hiyo katika mikoa 12 na kuona watu 7,196, ambapo 847 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.

Ofisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Farajiakitoa elimu ya jinsi ya kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo kwa kufuata mtindo bora wa maisha kwa wananchi waliofika katika kambi maalumu ya siku mbili ya matibabu ya moyo   jana JKCI Hospitali ya Dar Group.

Ofisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Dar Group, Ibrahim Amir akimpima uzito na urefu mwananchi aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.


 Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wakitoa ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo na lishe bora kwa wananchi waliofika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.

Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wakitoa ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo, matumizi sahihi ya dawa za moyo na lishe bora kwa wananchi waliofika JKCI Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana jijini Dar es Salaam.

Watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) makao makuu na Hospitali ya Dar Group wakichukuwa taarifa za wananchi waliofika katika Hospitali ya Dar Group kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),  Hospitali ya Dar Group, Flaviana Masegesa na Ofisa Masoko wa Hospitali hiyo, Ireen Mbonde , wakichukuwa taarifa mbalimbali wakati wa zoezi la uchunguzi na matibabu ya moyo lililomalizika jana katika Hospitali hiyo. Picha zote na JKCI

No comments